Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amezitaka Wizara na Taasisi husika kuhakikisha kuwa wabunifu katika sekta ya kilimo wanatambuliwa na kulindwa kisheria ili waweze kunufaika.
Mhe. Mpango ametoa agizo hilo tarehe 1 Agosti, 2023 alipokuwa akifungua Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima (Nanenane) yanayofanyika katika Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Mhe. Mpango amesema yanapofanyika maonesho haya ni muhimu kuwatambua wabunifu katika sekta ya kilimo, mifugo na Uvuvi ikiwa ni njia mojawapo ya kuwahamasisha na kuwasaidia kulinda ubunifu wao kisheria.
“Nimefurahi kumuona mbunifu ambaye ameunda gari inayopukuchua mahindi na bidhaa zingine,
mbunifu kama huyu anapaswa kusaidiwa ili anufaike na ubunifu wake”, amesema Mhe. Mpango.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi katika ufunguzi wa maonesho hayo Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe amesema umefika wakati sasa kwa bidhaa zote za chakula na mbegu kutoka Tanzania kwenda nje ya nchi zitambulike kwa kuhusisha masuala ya Miliki Ubunifu tofauti na ilivyo sasa.
Amesema Tanzania ina utajiri wa mazao mengi ya chakula pamoja na mbegu bora zilizofanyiwa utafiti na vituo vya Utafiti vilivyopo nchini lakini vinaposafirishwa nje ya nchi havitambuliki kama asili yake ni Tanzania hivyo suala la miliki ubunifu ni muhimu kukulizingatia.
Wakala wa Usajili wa Biasahara na Leseni (BRELA) ambayo inashiriki katika maonesho hayo, mbali na kuhamasisha urasimishaji wa biashara pia itatumia fursa ya maonesho hayo kuwatembelea wabunifu mbalimbali ili kuwapatia elimu kuhusu usajili wa Vumbuzi zao BRELA ili waweze kulindwa kisheria.
Katika maonesho hayo yatakayohitimishwa tarehe 8 Agosti, 2023, yenye kauli mbiu ‘Vijana na wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula’, BRELA inatoa huduma za papo kwa papo za sajili na elimu kwa wadau wanaotembelea mabanda yake.