Mkurugenzi Mtendaji wa bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu CPA ,Pius Maneno akizindua kozi hizo katika chuo cha Uhasibu Arusha ,pembeni yake ni Mkuu wa chuo cha Uhasibu Arusha, Prof. Eliamani Sedoyeka.
Mkurugenzi Mtendaji wa bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu ,CPA Pius Maneno akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo katika chuo cha uhasibu Arusha
Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha ,Prof.Eliamani Sedoyeka akizungumza katika uzinduzi huo jijini Arusha leo.
Julieth Laizer, Arusha .
Arusha .MKURUGENZI Mtendaji wa Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) CPA Pius Maneno amewataka wahasibu na wakaguzi nchini kuwa na mazoea ya kufanya ukaguzi wa miradi inayotekelezwa na serikali kwa vitendo mara kwa mara ili kuleta matokeo chanya na thamani halisi ya fedha.
Ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akizindua Shahada ya Uhasibu na fedha pamoja na Shahada ya ukaguzi wa hesabu na uhakikisho katika chuo cha uhasibu Arusha na kusisitiza wataalamu kujenga nidhamu,misingi na weledi sanjari na kuendana na mabadiliko ya teknolojia.
Amesema kuwa,serikali inatumia fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ila changamoto iliyopo ni kuwepo kwa mazoea katika usimamizi wa miradi hiyo kutokana na kufanyiwa ukaguzi mwishoni jambo ambalo limekuwa likichangia kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha ,hivyo kutaka miradi kufanyiwa ukaguzi wakati ikiendelea ili penye mapungufu paweze kurekebishwa.
“kitendo cha chuo hicho kuanzisha mitaala hiyo kitasaidia sana kupata wataalamu waliobobea katika eneo la fedha na ukaguzi ambao wataweza kufanya vizuri katika utendaji kazi wao na kusimamia suala la thamani ya fedha za miradi wanayosimamia katika utendaji kazi wao wa kila siku” amesema CPA Maneno.
Amesema kuwa,shahada hizo zitakuwa na mchango mkubwa katika kuongeza wataalamu watakaosimamia matumizi ya fedha hapa nchini, na ambao watasaidia kukagua hesabu na kuhakikisha fedha zimetumika kwa malengo yaliyokusudiwa kwa manufaa ya mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Aidha ametoa wito kwa wadau wote wenye sifa kwa hapa nchini na nchi nyingine kuchangamkia fursa hiyo kujiunga na programu hizo ambazo zinatarajiwa kuanza kutolewa chuoni hapo katika mwaka huu wa masomo, ili kuweza kupambana na soko la ajira lililopo ndani na nje ya nchi kutokana na uhitaji mkubwa uliopo wa wataalamu hao.
“Kitendo cha chuo hiki kuanzisha programu hii mpya ni jambo zuri sana na linapaswa kuigwa kwani tayari kuna soko la uhakika ndani na nje ya nchi kutokana na wataalamu hao kuhitajika katika nchi mbalimbali ,hivyo nawaombeni sana watanzania wachangamkie fursa hiyo. “amesema CPA Maneno.
Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha,Prof .Eliamani Sedoyeka akizungumza katika hafla hiyo amesema kuwa,chuo hicho katika mwaka wa masomo 2023/2024 tunatarajia kuanzisha kozi mpya tano ambapo kati ya hizo kozi za shahada ni nne na moja ya shahada ya Uzamili.
Amesema kuwa, kozi hizo wanazotarajia kuanza mwaka huu zinazingatia mahitaji yaliyopo sokoni kwani wamekuwa wakifanya tafiti mbalimbali kwa lengo la kufahamu mahitaji halisi ya watanzania na serikali kwa ujumla na hivyo zitaweza kukidhi soko la Afrika Mashariki na nchi za SADC
Kwa upande wake Mkurugenzi kutoka kampuni ya Auditax International ,CPA Josina Tarimo amesema kuwa,chuo hicho kimelenga mahitaji ya soko kwani kuna fursa kubwa ya kupata ajira ndani na nje ya nchi kupitia kozi hizo kwani wanahitajika wataalamu waliobobea na wenye uzoefu katika maswala hayo.