Na. Mwandishi Wetu-DSM
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kimeshiriki Kongamano lililoandaliwa na Taasisi ya Africa India Business Organisation lililofanyika katika Hoteli ya Kilimanjaro Jijini Dar es Salaam Julai 29, 2023 ambako ilipata nafasi ya kueleza manufaa na fursa za uwekezaji zinazopatikana Tanzania kwenye sekta mbalimbali.
Akizungumza katika Kongamano hilo, Afisa Uwekezaji kutoka TIC, Bi. Elizabeth Muzo alisema kuwa wawekezaji wanakaribishwa Tanzania kwani kuna mabadiliko makubwa katika sekta ya uwekezaji ambayo yanawapa uhakika wa kuwekeza nchini.
“ Tumepata Fursa ya kushiriki Kongamano hili ambalo limeandaliwa na wenzetu wa Africa India Business Organisation, Sisi TIC tumewaeleza washiriki wa Mkutano huu kuwa kuna fursa nyingi za uwekezaji, lakini tumewaeleza huduma zinazotolewa na Kituo chetu cha uwekezaji pamoja na Mabadiliko ambayo yameletwa na Sheria Mpya ya Uwekezaji ya mwaka 2022”, Aisema Bi. Muzo.
Bi. Muzo alisema kuwa washiriki na wawekezaji walioshiriki Mkutano huo walifurahishwa na Habari za mabadiliko ya Sheria ya Uwekezaji ya Mwaka 2022, na kusema watakuja kuwekeza nchini ili kupata faida na kukuza mitaji yao.
Aidha, Bi. Muzo alisema kuwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania, kinahudumia wawekezaji kwa haraka kupitia huduma ya mahala pamoja ambayo inajumlisha Taasisi 12 za Serikali ambazo zipo TIC zinatoa huduma na kuharakisha michakato ya uwekezaji nchini.