Angela Msimbira TABORA
MAOFISA Elimu Kata wameagizwa kuhakikisha shule zote wanazoziongoza zinatumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika ufundishaji na ujifunzaji ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Elimu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Vicent Kayombo ametoa agizo hilo Julai 30, 2023 mkoani Tabora alipokuwa akifunga mafunzo ya matumizi bora na salama ya vifaa vya TEHAMA na vishikwambi kwa walimu wa shule za awali na msingi Tanzania Bara.
Kayombo amesema Serikali imeamua kujikita katika kuhakikisha inaboresha ufundishaji na ujifunzaji kwa njia ya TEHAMA hivyo mnajukumu la kuleta mabadiliko katika maeneo yao.
“Tunatarajia afisa elimu wa Kata aliyepata mafunzo kuhakikisha kwenye kata yako walimu wote wanapata mahiri wa kutumia vifaa vya TEHAMA kwa kuhakikisha mnakuwa mfano katika kutenda na kuelekeza, tukikuta kwenye kata yako hakuna mabadiliko hatua zitachukuliwa,” amesema Kayombo
Amesema kuwa Serikali imebeba jukumu kubwa la kuboresha ufundishaji na ujifunzaji kwa njia ya TEHAMA, hivyo Maafisa elimu kata wanawajibu wa kuhakikisha wanakuwa mfano bora wa kutumia vifaa vya TEHAMA mashuleni
Amewataka Maafisa Elimu Kata kutumia programu ya MEWAKA kuwawezesha walimu wengine katika shule na kata ili kuwa na uelewa wa pamoja juu ya matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji shuleni huku akiwahimiza kuandaa mpango kazi wa namna ya kutekeleza mafunzo ya TEHAMA kwa walimu wengine.
Naye, Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Mafunzo ya Ualimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Huruma Mageni amewataka kuhakikisha wanatumia teknolojia katika kufundisha na kujifunzia ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani.