Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Ndugu Daniel Chongolo akihutubia maelfu ya wana CCM na wananchi walionitokeza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Tanganyika Pakers Kawe jijini Dar es Salaam leo Julai 29,2023.
……………………………….
Na John Bukuku,Dar es Salaam
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kinachofanywa na Serikali katika suala la bandari ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo inatakiwa ifikapo mwaka 2025 mambo yote yawe yametekelezwa.
Akizungumza leo Julai 29,2023 wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Tanganyika Pakers, Dar es Salaam na kuhudhuriwa pia na viongozi wa Mikoa ya Pwani na Morogoro, Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, amesema
Amesema dhamira ya CCM ni kuhakikisha kinapata fedha za kutosha kwenye kila chanzo cha muhimu ili zisaidie kuharakisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi.
“Sasa hofu yetu nini, kwanini watu hawataki tuje, tukae, tupitie, tujadiliane, tupate maeneo ambayo tunafikiri yana tija zaidi tuyarekebishe…wanapita wanatukana.
“Maana yake ajenda sio tija au marekebisho ya mkataba, tutakuwa watu wa ajabu sana, tumepewa dhamana ya kuongoza nchi hii, sisi ndio tumeshika usukani ni lazima tuonyeshe ukomavu wa kuendesha gari lifike linakotakiwa…wasiwe na wasiwasi wajue kwamba tuliokalia kiti tunajua wajibu wetu, dhamana zetu, na tunajua namna ya kuzitafsiri zitendewe haki.
“Amani hii ina historia, ina mizizi iliyojikita na walioiasisi hawapo, wameturithisha, tusiwarithishe watoto wetu damu, chuki, uadui kwa sababu tutakuwa hatujatimiza wajibu wetu na tutakuwa tumeondoka kwenye mstari ulioasisiwa na waasisi wetu…laana na hukumu hiyo hatutaikwepa,” amesema Chongolo.
Mwanasiasa Mkongwe, Stephen Wasira, akizungumza katika mkutano huo amehoji nani atakayeuza bandari akabaki na akili timamu na kusema bandari ni mpaka kati ya nchi yetu na nyingine.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Jerry Silaa, amesema miradi inayotajwa iko saba na hakuna mradi wowote ulioanza wa uwekezaji wa bandari hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo, amesema uwekezaji huo ni muhimu kwani una manufaa kwa taifa na Watanzania.
“Niwahakikishie Serikali haiwezi kuuza bandari na bandari haiuziki, wanaosema uwekezaji uendelee lakini baadhi ya vipengele katika mkataba viangaliwe. Serikali haina tatizo na wataalam na Watanzania wenye nia njema,” amesema Profesa Mkumbo.