Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amewataka waumini na dini ya kiislam na wananchi kuendelea kudumisha Umoja na Mshikamano uliopo ili kuendelea kutunza Amani iliyopo kwa maslahi ya vizazi vya sasa na baadae.
Akiwasalimia waumini wa Masjid Maryam Mtoni Kidatu katika Ibada ya Sala ya Ijumaa, Alhajj Hemed amesema ni jukumu la kila Mzanzibari kuhakikisha nchi inabaki kuwa salama muda wote ili kuiwezesha Serikali kutekeleza mipango ya maendeleo kwa Wanachi wake.
Aidha, Alhajj Hemed amesema Umoja na mshikamano uliopo umewezesha jamii kuishi kwa Amani,upendo na mshikamano pamoja na kuimarika kwa ustawi wa jamii.
Sambamba na hayo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka Wananchi kujivunia hatua za maendeleo zilizofikiwa katika miradi mbali mbali ya miundombinu na mawasiliano katika kuwatatulia changamoto mbali mbali zinawakabili.
Pia Mhe, Hemed amewataka baadhi ya viongozi kuacha tabia ya kuwapotosha wananchi juu ya Maendeleo yanayofanywa na Serikali jambo ambalo linaweza kuwaletea kutokuelewana baina yao. kufanya hivyo ni kuchukua jukumu kubwa kwa Mwenyezimungu ambapo watakwenda kuulizwa mbele ya haki.
Kadhalika, amewataka wazazi na walezi kuwawekea mazingira mazuri vijana wao pamoja na kuwasimamia katika malezi na kudumisha Ibada ili kuweza kuishi Kwa Amani na upendo pamoja na kutarajia malipo mbele ya haki.
Akitoa Khutba ya Sala ya Ijumaa Sheikh Ali Juma Mwazini amewataka Waislamu kuzidisha kumcha Mwenyezi ili kufikia sifa za watu wa peponi katika kutoa kile ambacho Mwenyezi Mungu amewaruzuku kwa njia iliyo sahihi ili kutarajia Pepo siku ya kiyama.
Aidha Sheikh Mwazini amewataka waumini kuacha kufanya maasi pamoja na Yale yote yanayomkirihisha Mwenyezi Mungu ili kuweza kuishi kwa Amani na upendo miongoni mwao.