Waziri wa ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi Dkt.Angelina Mabula akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya jengo la Ofisi ya Serikali ya mtaa wa kilimahewa kata ya Nyamanoro Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza.
Muonekano wa jengo la Ofisi ya Serikali ya mtaa wa kilimahewa iliyojengwa kwa nguvu za wananchi pamoja na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angelina Mabula.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angelina Mabula amesema ili kuondokana na migogoro ya ardhi ni vema kila mwananchi ahakikishe ana hati miliki ya eneo lake.
Dkt.Mabula ameyasema hayo leo Julai 28, 2023 alipokuwa kwenye ukaguzi wa maendeleo ya jengo la Ofisi ya Serikali ya mtaa wa Kilimahewa ‘A’ iliyopo Kata ya Nyamanoro Wilaya ya Ilemela Mkoani hapa ambapo ni sehemu moja wapo ya ziara yake ya kikazi ya kutembelea Kata zote kwaajili ya kukagua miradi inayotekelezwa kwenye Jimbo hilo.
“Nasisitiza maeneo yote ambayo yalitengwa kwaajili ya umma yanatakiwa kuwa na hati miliki ili mipaka ijulikane na yasiingiliane na watu ili kuepusha migogoro”, amesema Dkt.Mabula.
Ameeleza kuwa ugomvi wa migogoro ya ardhi inatokea mara nyingi kwasababu ya kutojua mipaka,eneo linakuwa limetengwa kwaajili ya matumizi ya umma lakini watu wengine wanaingia wanajenga hadi kwenye kiwanja kwasababu hakuna mipaka inayoonekana hivyo ili uwe na salama kwenye eneo lako ni lazima uwe na hati miliki.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Kilimahewa ‘A’ Amini Fataki, amesema ofisi hiyo imejengwa kwa nguvu za wananchi pamoja na Mbunge wa jimbo hilo.
” Ujenzi wa jengo hili kwa sasa umefikia kwenye hatua ya kupaua ambapo wananchi walichangia elfu mbili mbili kila kaya na Mbunge kupitia mfuko wa Jimbo akachangia mifuko 10 ya Saruji na matofari 700″, amesema Fataki.