Meneja Mahusiano na Mawasiliano wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Bw Yessaya Mwakifulefule akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania TCAA kuhusu zoezi la utafutaji na uokoaji wa ndege uliofanyika leo Alhamisi Julai 27,2023 jijini Dar es Salaam, kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma za Uongozaji Ndege TCAA Bi. Flora Mwanshinga.
……………………………
Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania TCAA imetoa taarifa kuhusu zoezi la utafutaji na uokoaji wa ndege ya abiria iliyoanguka katika kijiji cha Msufini Kidete, Kata ya Mbezi, tarafa ya Shungubweni, wilaya ya Mkuranga, mkoa wa Pwani ikiwa inatoka katika uwanja wa Kilwa Masoko na kuelekea uwanja Tanga.
Ndege hiyo aina ya Embraer 120 (E120) ilikuwa imebeba abiria 25.
Natoa taarifa kwamba kilichofanyika leo ilikuwa ni zoezi ambalo lengo lake ni kupima uwezo na utayari wetu kama nchi wa kukabiliana na matukio ya utafutaji na uokoaji wa ndege zinazopata ajali kwenye nchi kavu au majini na pia nyombo vya majini.
Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya Mamlaka ya hiyo Meneja Mahusiano na Mawasiliano wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Bw Yessaya Mwakifulefule amesema zoezi hilo limeandaliwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), ambayo inajukumu la kuratibu na kusimamia huduma ya utafutaji na uokoaji wa ndege zinazopata ajali kwenye anga la Tanzania.
Mwakifulefule amesema TCAA imeshirikiana na Taasisi za udhibiti wa usafiri wa majini ambayo ni Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa Tanzania bara na Mamlaka ya Usafiri wa Baharini (ZMA) kwa upande wa Zanzibar.
Amefafanua kuwa zoezi hilo pia limehushisha taasisi za utafutaji na uokoaji za umma na binafsi kama Jeshi la Wananchi (JWTZ), Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mashirika ya ndege, Mashirika ya vyombo vya majini, Mamlaka ya viwanja vya ndege (TAA), Mamlaka ya hali ya hewa (TMA), Hospitali, Shirika la msalaba Mwekundu Tanzania (Red Cross), Wavuvi, pamoja wadau wengine mtambuka wa utafutaji na uokoaji.
Kauli mbiu ya zoezi la mwaka huu 2023 ni “Okoa Maisha” (Save life). Ambapo
Tanzania iliridhia Mkataba wa Kimataifa wa Usafiri wa Anga (ICAO Convention) mwaka 1962 na Mkataba wa Shirika la Bahari Duniani (IMO) mwaka 1974 na kuwa mwanachama wa mashirika ya ICAO na IMO.
Mkataba wa Kimataifa wa Usafiri wa Anga wa mwaka 1944 ulioridhiwa una kiambatisho Na. 12 (Annex 12) ambacho kinaelezea kuhusu masuala ya utafutaji na uokoaji.
Kadhalika Mwakifulefule ameongeza kuwa Tanzania imeridhia Mkataba wa Kimataifa wa Utafutaji na Uokoaji Majini wa mwaka 1979 (International Convention on Maritime Search and Rescue, (SAR Convetion,1979) unaozungumzia kuhusu masuala ya utafutaji na uokoaji katika usafiri wa majini.
Ametanabaisha kuwa mikataba hiyo yote inayosimamiwa na ICAO na IMO inazitaka nchi wanachama kutoa huduma za utafutaji na uokoaji katika usafiri wa anga na majini wakati ajali na matukio ya dharura ya vyombo vya usafiri wa anga na majini ndani ya eneo la nchi mwanachama yanapotokea .
Kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, eneo la nchi la utafutaji na uokoaji ni mipaka ya kimataifa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na eneo la Bahari ya Hindi kuanzia pwani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuelekea Mashariki hadi Longitudi nyuzi 44 (440E) pamoja na maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.
Mwaka 1999, ICAO na IMO ziliandaa Mwongozo wa pamoja wa Utafutaji na Uokoaji katika Usafiri wa Anga na Majini (International Aeronautical and Maritime Search and Rescue (IAMSAR) Manual) ambao ulianza kutumika mwaka 2001.
Ameongeza kuwa lengo kuu la mwongozo huo ni kuweka utaratibu wa pamoja wa utafutaji na uokoaji wakati wa ajali na matukio ya dharura ya usafiri wa angani na majini.
Katika utekelezaji wa maelekezo yaliyo katika Mwongozo huo, Tanzania imeimarisha na kuboresha vituo vya kuratibu shughuli za utafutaji na uokoaji katika usafiri wa anga na majini.
Vituo hivyo vinavyojulikana kama Aeronautical Rescue Coordination Centre (ARCC) ambacho kipo katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam na Maritime Rescue Coordination Centre (MRCC) ambacho kipo eneo la Magogoni, Dar es Salaam. Kituo cha ARCC kinasimamiwa na TCAA na kituo cha MRCC kinasimamiwa na TASAC.
Miongoni mwa maelekezo muhimu yaliyoko katika mwongozo huo ni pamoja na kuzitaka nchi wanachama kuwa na Mpango wa Kitaifa wa kuratibu shughuli za Utafutaji na Uokoaji katika usafiri wa anga na majini (National Aeronautical and Maritime Search and Rescue Plan). Mwongozo huo wa ICAO na IMO pia huzitaka nchi wanachama kuufanyia majaribio au mazoezi mpango huo ili kupima uwezo na utayari wa taasisi zote zinazohusika katika kutoa huduma hii muhimu ya utafutaji na uokoaji.
Hivyo kufanya mazoezi haya ni kutekeleza matakwa ya sheria na mikataba ya kimataifa ili kuboresha mifumo, taratibu na vifaa vya utafutaji na uokoaji.
Zoezi hili limehusisha waangalizi wa ndani na nje ya nchi ili kutathmini maeneo yanahitaji kuboreshwa ili huduma hii itolewe kwa ufanisi mkubwa.
Waangalizi hao ni kutoka Shirika la kimataifa la usafiri wa anga duniani (ICAO), Mashirika ya ndege ya ndani na nje ya nchi, Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) na Mashirika ya vyombo vya majini.
Waangalizi hawa watatoa ripoti ambazo zitafanyiwa kazi ya kamati ya kitaifa ya utafutaji na uokoaji wa ajali za ndege na vyombo vya majini.
Mwisho, nichukue nafasi hii tena kuwashukuru Waandishi wa habari wote kwa kuhudhuria mkutano huu.