Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (Bara) Ndg. Abdulrahman Kinana akipeana Mikono na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga alipowasili Mkoani humo kwa Ziara ya Kukagua Uhai wa Chama Na Kukagua Maendeleo ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020 – 2025 Leo. (Picha na Fahadi Siraji CCM)
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulrahman Kinana amesema hakuna sababu ya wananchi kubadilisha viongozi kama mashati kwani kufanya hivyo kunarudisha nyuma maendeleo.
Akizungumza wilayani Kondoa mkoani Dodoma wakati wa mkutano wa hadhara uliondaliwa na Mbunge wa Jimbo la Kondoa Dk. Ashatu Kijaji kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, Kinana alitumia nafasi hiyo kuzungumzia umuhimu wa wananchi kujenga tabia ya kutobadilsha viongozi wao kama mashati kama hakuna ulazima wa kufanya hivyo.
Kinana alisema kila binadamu ana kasoro, hakuna mkamilifu, lakini wamamchi hususan wapigakura wasimwadhibu mtu kwa mambo madogomadogo, badala yake waangale mambo makubwa na mazuri anayoyafanya huku akitoa mfano kuwa majimbo yote ambayo wabunge wake hawabadilishwi kama mashati hupiga hatua kubwa za maendeleo.
“Ilani yetu ya uchaguzi ina kurasa 303 lakini kitabu hiki (kinachoonyesha utekelezaji wa Ilani) katika jimbo la Kondoa kwa kipindi cha miaka miwili na nusu, kuna kurasa 100 zinazoelezea jimbo la Kondoa Vijijini mambo ambayo yamefanyika. Ni kweli serikali imefanya makubwa, vile vile kuna mtu ambaye ni kiungo kati ya serikali kuu, Halmashauri, Chama Cha Mapinduzi na Bunge naye ni mbunge,” alisema.
Alifafanua kuwa inawezekana mbunge asifanye kila kitu ni binadamu na anaweza kuwa na kasoro, lakini ukitaka kuishi na mwenzako vizuri tafuta mema yake usitafute upungufu wake.
“Wote tunavyoishi ukitafuta upungufu wa mtu mtakosana ukizungumza mema yake mtaishi pamoja kila binadamu anaupungufu wake hata mimi nina yangu. Na yeye atakuwa anajua upungufu wao lakini yote yanawekwa kando na kutafuta mema na kufanya maisha kuwa mazuri,” alisema.
Aidha, alisisitiza katika kufanikisha maendeleo yoyote ni lazima kuwepo umoja na mshikamano, kwani mambo hayo yasipokuwepo maendeleo yatakuwa hafifu kwa sababu viongozi na wananchi watakuwa wakibisha katika kila jambo.
“Mnataka kuweka mradi wa maji mnabishania mradi uende wapi, mnataka kujenga shule mnasema ijengwe wapi, mnabishana hadi fedha zinarudi serikali kuu. Mnataka kuamua nyumba za walimu zijengwe wapi hamkubaliani. Mkiwa na umoja maendeleo yatakuwa yaharaka zaidi.
“Mkitaka kuamua fedha tulizonazo za ujenzi wa barabara ni ndogo tuanze na barabara ipi mkavutana mtaendelea kubishana hadi hapo fedha zitakapokuwa zimerudi serikali kuu. Kila ifikapo Juni serikali inatafuta fedha zote ambazo hazikutumika zinarudishwa katika hazina kuu ya serikali, niliwahi kuwa mbunge na hilo nalijua.
“Kwa hiyo hakikisheni kila fedha iliyotengwa fedha zote zinatumika kwa yale yaliyokusudiwa lakini vile vile kwa miradi iliyokusudiwa.
“Ni vema ikafahamika kuwa kiongozi hawezi kufanya kazi wala kuleta maendeleo peke yae bali na wananchi wote kwa ujumla wao,” alisema,