Dodoma,
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesikitishwa sana na kinalaani vikali tukio la kushambuliwana, kujeruhiwa na kuporwa mali Wanahabari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), lililotokea Julai 22, 2023, maeneo ya Temeke, mkoani Dar es Salaam, wakati waandishi wa habari wa chombo hicho, walipokuwa wakitekeleza majukumu yao.
Pamoja na kukemea vikali kitendo hicho ambacho ni uvunjifu wa sheria za nchi yetu, Chama Cha Mapinduzi kinatoa wito kwa vyombo vya dola, kuwasaka na kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika kuwashambulia, kuwajeruhi, kuwapora mali au vitendea kazi waandishi wa habari hao, na kuharibu mali za kampuni hiyo, hususan gari walilokuwa wakitumia katika kazi zao.
Mbali ya kuwapatia pole waandishi hao, Fortune Francis na Sunday George pamoja na dereva wa gari Omary Mhando, CCM ikiwa mdau wa uhuru wa habari, tasnia ya habari na vyombo vya habari nchini, inatoa wito kwa jamii kutambua, kuheshimu na kulinda uhuru wa wanahabari ambao wana wajibu mkubwa wa kutoa habari, kuburudisha na kuelimisha jamii juu ya masuala mbalimbali, yakiwemo yanayohusu maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Wakati huo huo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinatoa salaam za rambirambi na pole kufuatia taarifa ya kuhudhunisha ya vifo vya watu 6 na majeruhi 16, vilivyotokea baada ya ajali mbaya ya gari iliyowagonga Wana-mazoezi wa Kikundi cha Hoteli ya Edden, waliokuwa wakifanya mazoezi kandokando ya barabara eneo la Sabasaba – Kiseke, Ilemela, mkoani Mwanza, Jumamosi Julai 22, 2023.
Chama Cha Mapinduzi kinatoa wito kwa vyombo vinavyohusika kusimamia usalama wa raia na mali zao, zikiwemo sheria za usalama barabarani kuendelea kuwaelimisha watumiaji mbalimbali wa barabara ili wachukue tahadhari zote za kulinda usalama wao na wengine, kwa kuzingatia taratibu za kisheria wawapo barabarani, sambamba na kuwachukulia hatua kali wakosaji wote, hasa wanaoendesha kasi, na kusababisha vifo, majeruhi majonzi na hudhuni kubwa kwa jamii kwa kupoteza wapendwa wao, kusababisha maumivu, ulemavu na kupoteza nguvu kazi katika ngazi ya mtu mmoja mmoja, familia, jamii na taifa letu kwa ujumla.