WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaasa Watanzania watambue kuwa utulivu, amani, umoja na mshikamano ndiyo nguzo muhimu katika ustawi wa Taifa kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Ametoa wito huo leo (Jumapili, Julai 23, 2023) wakati akizungumza na washiriki wa Kongamano la Mafunzo ya Shirikisho la Kimataifa la Polisi Wanawake (IAWP) Kanda ya Afrika lililofanyika kwenye uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu ambaye amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi wa kongamano hilo, amesema: “Uhuru huu wa mawazo tulionao hapa nchini unatolewa kikatiba. Na pia uhuru tulionao unaenda na wajibu. Watu wasisahau kuwa umoja wa nchi umejengwa siku nyingi. Kwa hiyo tusitamani kuuharibu kwa manufaa ya watu wachache,” amesisitiza.
Amewataka washiriki wa kongamano hilo, wakawe chachu ya mabadiliko katika utendaji kazi na wawe mfano kupitia maarifa mapya watakayoyapata. “Nendeni mkawashirikishe wenzenu ambao hawajapata fursa ya kushiriki katika mafunzo haya ili wote kwa pamoja mpate manufaa ya Tanzania kuwa mwenyeji wa kongamno hili la mafunzo.”
Kuhusu umuhimu wa mafunzo, Waziri Mkuu amesema: “Askari wa kike, changamkieni fursa za mafunzo ya taaluma adimu ndani ya Jeshi la Polisi, na hii ni namna bora ya kuongeza uwakilishi wa wanawake katika kila idara ndani ya jeshi.”
Katika kongamano hilo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitunukiwa tuzo maalum kwa kutambua na kuthamini mchango wa askari wa kike nchini na kuwaamini kushika nafasi mbalimbali za uongozi.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki hao, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni amesema Tanzania iko salama chini ya usimamizi wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF Net), Kamishna wa Utawala na Rasilmali Watu wa Jeshi Polisi, Suzan Kaganda alisema mtandao huo ulianzishwa Oktoba, 2007 ili kuongeza ubunifu miongoni mwa wanachama wake na kuongeza tija ya utoaji huduma kwa jamii.
“Kupitia mtandao huu, madawati 420 yameanzishwa kwenye vituo vya polisi kote nchini ambapo tumeweza pia kuanzisha madawati 79 ya kisasa kupitia kwa wadau. Madawati hayo yametumika kutoa elimu na kuwezesha kuzuia makosa ya unyanyasaji wa kijinsia katika jamii.”
Amesema siku hizi watu wanatoa taarifa za mara kwa mara ikilinganishwa na hapo zamani na kwamba wanatoa huduma kwa watoto na wanaume. ‘Wanaume wasisite kutayumia madawati hayo pindi wanapopata changamoto,” amesisistiza.