Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Kutokana na juhudi mbalimbali za kukuza maendeleo ya nchi zinazofanyika nchini Tanzania kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, afya, miundombinu, uwekezaji, viwanda, kilimo na utalii n.k, Tanzania imeendelea kuonekana duniani na kuwa nchi ya mfano.
Wakati akizindua mchakato wa maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika, Kuhusu Maendeleo ya Rasilimali Watu mnamo mwezi Mei, 2023, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema kuwa, kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa inaonesha kuwa nchi za Afrika zinakabiliwa na changamoto ya kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) zinazohusiana na maendeleo ya rasilimali watu japo Tanzania imeanza kuchukua hatua na inaendelea vizuri.
“Tanzania tayari tumeshaanza kuchukua hatua mbalimbali katika kutekeleza SDGs na tunasonga mbele”, alisema Rais Samia.
Hatua hizo za kimaendeleo zinazopigwa na nchi ya Tanzania ndizo zilizopelekea Benki ya Dunia (World Bank) kuamua kufanyia mkutano mkubwa na wa kwanza Afrika unaokutanisha Wakuu wa Nchi za Afrika kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali yanayohusu Rasilimali Watu.
Baadhi ya hatua hizo ni katika suala la elimu ambapo Serikali imeweka mazingira bora ya elimu yatakayosaidia kuandaa wataalam bora na wengi zaidi kwa kutoa elimu bila malipo kuanzia shule ya awali hadi kidato cha sita pamoja na Vyuo vya Ufundi, imeweka utaratibu wa wanafunzi kupata mikopo kuanzia ngazi ya Vyuo vya Kati na kuongeza takribani mara mbili ya fedha za mikopo ya Elimu ya Juu pamoja na kuongeza posho za wanafunzi.
Vilevile, Serikali imeamua kuwekeza katika uchumi wa kidijitali kwa kuwekeza katika mafunzo hayo ambapo itajenga chuo kikubwa cha masuala ya TEHAMA ili kuhakikisha kuwa uchumi huo unapewa msukumo mkubwa.
Uwepo wa usalama, amani na utulivu kwa nchi ya Tanzania pia umechangia mkutano huu kufanyikia hapa nchini. Aidha, uwepo wa vijana wa kutosha ambao ndio nguvu kazi ya Taifa utawasaidia nchi washiriki kujifunza namna Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyopambana na changamoto ya ajira kwa vijana.
Mkutano huu umeweka historia na heshima kwa nchi ya Tanzania kwani Jiji la Dar es Salaam ndilo litatumika kuandaa Azimio la Dar es Salaam juu ya rasilimali watu, pia uwepo wa mkutano huu utasaidia kukuza uchumi wa nchi na kuongeza kipato kwa mwananchi mmoja mmoja.
Wageni hawa mbali na fursa hii ya utalii wa mikutano, pia watapata fursa ya kufanya utalii katika maeneo yetu mbalimbali ya utalii ikiwemo maeneo ya mbuga, fukwe, vyakula na Utamaduni.
Zaidi ya watu 1,200 kutoka nchi mbalimbali za Afrika wakiwemo Wakuu wa Nchi hizo, viongozi wa Serikali, Watumishi wa Umma, wadau, Waandishi wa Habari pamoja na wananchi wanatarajiwa kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali Watu utakaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Julai 25 hadi 26, 2023.
Mkutano huo utazungumzia masuala ya rasilimali watu hususan kwa vijana ambapo Sekta ya Elimu, Afya, Kilimo, Fedha na Sayansi na Teknolojia zitajadiliwa kama wazalishaji wa rasilimali watu.
Kwa siku ya kwanza mkutano utakutanisha Mawaziri ambapo pamoja na mambo mengine watatoa mapendekezo kuhusu azimio ambalo linatarajiwa kupitishwa siku ya pili ya mkutano huo ambao utahusisha Wakuu wa Nchi.
Mkutano huo pia haujawaacha nyuma wajasiriamali ambapo kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila amesema kuwa, zaidi ya wajasiriamali 120 wa ndani watapata fursa ya kuonesha na kuuza bidhaa zao wakiwemo wafanyabiashara wadogo.
“Wajasiriamali hao wameandaliwa mabanda maalumu takriban 100 kando ya barabara kuelekea ukumbi wa JNICC ambayo yamesambazwa katika sehemu mbalimbali za karibu na ukumbi huo ikiwemo katika eneo la barabara ya IFM ilipokuwa Wizara ya Fedha zamani.” Alimalizia Mhe. Chalamila.
Mpaka sasa maandalizi yamekamilika kwa asilimia 100 na wageni kutoka nchi mbalimbali wameanza kuingia akiwemo Rais wa Sao Tome, Mhe. Carlos Vila Nova ambaye tayari ameshawasili na kupokelewa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye.
Maandalizi ya ukumbi yamekamilika
Waziri wa Habari, Mawasiliana na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye akimpokea Rais wa Sao Tome, Mhe. Carlos Vila Nova, ambaye amewasili Nchi kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika Kuhusu Rasilimali Watu utakaofanyika Julai 25-26, 2023, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam.