Na Philipo Hassan, Kilimanjaro.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye (MB) leo tarehe 22.07.2023 amepokea msafara wa mashabiki kindakindaki wa timu ya mpira wa miguu ya Simba waliotoka kuzindua jezi mpya kwa ajili ya msimu wa 2023/2024 unaotarajia kuanza mapema mwezi Agosti 2023 katika Kilele cha Mlima Kilimanjaro, mapokezi yaliyofanyika katika Lango la Marangu lililopo Mkoani Kilimanjaro.
Akiwa katika lango hilo Mhe.Nape aliwapongeza Simba SC kwa kuandika historia kubwa ambayo haijawahi kufanywa na timu yoyote ya Tanzania na Afrika kuzindua Jezi katika kilele kirefu zaidi barani Afrika chenye mita 5895 kutoka usawa wa bahari. Hata hivyo pia, alisema “kujitolea kwenu kumeonyesha uzalendo mlionao katika kuzionyesha na kuzitangaza maliasili zetu, nina uhakika kwa wale walioangalia mitandao yenu ya kijamii, ndani na nje ya nchi wameona mambo yenu”.
Aidha, Mhe. Nape alishuhudia jezi zenye majina ya viongozi wa nchi ambao ni Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kasim Majaliwa, Rais wa Zanzibar Dkt. Hussen Mwinyi.
Naye, Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa aliipongeza timu ya Simba kwa ubunifu huo wa kuvitangaza vivutio vyetu kwa njia ya Uzinduzi wa jezi na kuvitaka vilabu vingine kuiga mfano huo kwa kufanya matukio yanayofanana na hayo katika hifadhi za Taifa za Serengeti, Ruaha na Katavi.
Akiongea mbele ya vyombo vya habari, Msemaji Mkuu wa Klabu ya Simba Ahmed Ally, aliwapongeza mashujaa waliopeleka kibegi hicho katika kilele cha Mlima Kilimanjaro na kuwaalika mashujaa hao kushirika wiki ya Simba (Simba Day) jijini Dar es salaam. Pia, Ahmedy Ally aliishukuru Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro kwa mapokezi na huduma nzuri walizopewa kufanikisha tukio hilo la kihistoria kwa Tanzania.
Zoezi la upadishaji wa kibegi chenye jezi za Simba SC ulianza tarehe 19.07.2023 na kuhitimishwa leo katika Lango la Marangu ambapo jumatano jezi hizo zitauzwa kwa mnada, fedha zitakazopatikana zitatumika katika ujenzi wa Wodi ya mama na mtoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kibegi kilichotumika kitapelekwa katika Makumbusho ya Taifa Dar es Salaam kwa ajili ya kumbukumbu.