Wananchi wa Kijiji cha Rutoro Wilayani Muleba Mkoani Kagera wanaoishi kwenye Ranchi ya Kagoma wametakiwa kuhifadhi na kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji katika Sekta ya Maliasili na Utalii baada ya kumilikishwa ardhi.
Ameyasema hayo leo katika ziara ya Mawaziri wa Kisekta iliyolenga kutatua mgogoro wa Ranchi ya Kagoma Mkoani Kagera.
Amefafanua kuwa endapo wananchi watayatunza vizuri maeneo watakayopangiwa wataweza kuanzisha miradi ya Upandaji Miti, ufugaji nyuki na shughuli nyingine zitakazowasaidia kukuza uchumi wao.
“Ujumbe wetu ni kuhakikisha kwamba yale maeneo ambayo tutayahifadhi vizuri tutayatunza vizuri tuyafanye kuwa rasilimali za kesho kwa maendeleo ya kizazi cha sasa na baadae” Mhe. Masanja amesisitiza.
Aidha, amewaasa wananchi hao kuacha tabia ya kuvamia maeneo na badala yake wawe na mpango mzuri wa matumizi bora ya ardhi.
“Maisha ya kutangatanga yamepitwa na wakati mnatakiwa muwe na maeneo ya kuyahifadhi kwa ajili ya kuwapatia vipato na mengine yatakuwa kwa ajili ya shughuli za kibinadamu ” Mhe. Masanja amesema.
Kamati ya Mawaziri wa Kisekta imeridhia Halmashauri ya Wilaya ya Muleba kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi pamoja na kuwagawia wananchi maeneo mengine yaliyopangwa.