Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akizungumza wakati anafungua kikao cha mwaka cha kuwajengea uelewa wa sehemu ya pili ya Mapango wa kunusuru Kaya masikini kwa viongozi ngazi ya Mkoa na Wilaya uliofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Baadhi ya wadau ngazi ya Mkoa na Wilaya mkoani Ruvuma wakiwa kwenye kikao cha kujengewa uelewa wa sehemu ya pili ya Mpango wa kunusuru kaya masikini kilichofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.
……….
SERIKALI imetoa zaidi ya shilingi bilioni 33 kwa ajili ya kutekeleza mpango wa kunusuru kaya kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mkoani Ruvuma.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa TASAF katika kipindi cha pili kwenye mkutano wa mwaka 2022/2023 uliofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea,mratibu wa TASAF Mkoa wa Ruvuma Xsaveria Mlimira amesema serikali ilitoa kiasi hicho cha fedha katika Halmashauri zote kuanzia Julai 2020 hadi Juni 2023.
Hata hivyo amesema kati ya fedha hizo zaidi shilingi ya bilioni 30 zilitolewa kwa walengwa,shilingi bilioni 1.8 zilitumika kwa ajili ya ufuatiliaji ngazi ya Halmashauri na shilingi milioni 295.22 zilitumika kwa ajili ya ufuatiliaji ngazi ya vijiji.
“Lengo la mpango wa TASAF ni kuziwezesha kaya maskini sana kuongeza kipato,fursa na uwezo wa kugharamia mahitaji muhimu,Mkoa wa Ruvuma unatekeleza mpango huu ambao ulianza kutekelezwa katika Halmashauri ya Tunduru mwaka 2013’’,alisema Mlimira.
Akizungumzia utekelezaji wa miradi ya ajira za muda kwa kaya masikini,Mratibu huyo wa TASAF amesema mradi huo umelenga kutoa ajira kwa kaya masikini zenye watu wenye uwezo wa kufanya kazi kwa kushiriki katika kutekeleza miradi mbalimbali inayoibuliwa na jamii na kulipwa ujira.
Ameitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa visima vya asili,utengenezaji Barabara,ujenzi wa vivuko ambapo katika Mkoa wa Ruvuma hadi sasa miradi 663 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni nne imetekelezwa katika vijiji 649.
Akizungumza wakati anafungua mkutano huo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema kikao hicho kimelenga kuwajengea uelewa wa sehemu ya pili ya mpango wa kunusuru kaya masikini kwa viongozi ngazi ya Mkoa na wilaya.
Amesema Halmashauri zote zinatekeleza mpango wa kunusuru kaya masikini ambapo hadi kufikia Juni 2023 Mkoa ulikuwa na kaya 65,089 za walengwa zinazoendelea kunufaika na utekelezaji wa TASAF ambao upo katika sehemu ya pili ya utekelezaji.
Amesema mpango huo umekusudia kuongeza kipato,kuongeza rasilimali za lishe,kuongeza vitegauchumi na kuongeza upatikanaji wa huduma za afya,maji na elimu.
Amesema serikali kwa kushirikiana na wadau imewekeza fedha za kutosha katika utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini ambapo ameagiza Halmashauri zote kuhakikisha kuwa fedha hizo zinasimamiwa kikamilifu ili kuhakikisha zinaleta tija kwa jamii.
Amewaagiza wadau wote mkoani Ruvuma kutoa elimu kwa walengwa ili wafuzu kutoka katika kaya masikini na kaya nyingine masikini ambazo hazikuwa kwenye mpango huu ili ziweze kupata nafasi.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ameishukuru serikali kwa kuendelea kutoa fedha za utekelezaji wa kunusuru kaya masikini na kuwezesha kutekeleza miradi mingi ya TASAF.
Halmashauri zote nane mkoani Ruvuma zinatekeleza mpango wa kunusuru kaya masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF.