Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amewasihi Wananchi kutumia maneno ya staha pale wanapowasilisha hoja zao au kukosoa.
Waziri Nape ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam alipokuwa akizungumza katika Kongamano la majadiliano ya Ripoti ya Tume ya Haki Jinai lililohudhuriwa na Wataalamu, Viongozi Wastaafu, Watumishi wa Serikali na Wanafunzi.
Amesisitiza utamaduni wa Taifa la Tanzania ni kuheshimiana huku akitaka kukosoa kufanyike na maoni yatolewe bila ya kutoa lugha za matusi.
Waziri Nape amekumbusha maneno ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
kuwa watu washindane kwa hoja bila ya kupigana.
Pia amekumbusha kuwa mijadala ya Haki Jinai inapoendelea Watanzania wakumbuke kuwa Moyo wa Rais Samia Suluhu Hassan unataka Haki hivyo msingi wa yote ni watu watendewe haki.
Aidha, Waziri huyo wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari amesema tayari amezielekeza taasisi zilizo chini ya wizara yake kuandaa majukwaa mbalimbali kwa ajili ya kujadili na kuchambua mapendekezo hayo ya Tume ya Hali Jinai kwa lengo la kupata maoni ya Wananchi ili ubora upatikane