Uongozi wa Serikali wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro umeeleza kusikitishwa na Uamuzi wa mkandarasi kampuni ya Advent Contraction ya Dar es Salaam kusimama kazi na kuondoa Mitambo katika eneo la Mradi mkubwa wa Maji Same,Mwanga-Korogwe ikielezwa huenda hatua hiyo ikaathiri utekelezaji na kufanya mradi kushindwa kukamilika kwa wakati.
Mradi huo wa Muda mrefu unatekelezwa kwa awamu mbili, awamu ya kwanza ikitarajiwa kukamilika Julai ya mwakani 2024 wastani wa shilingi Bilion 137 zikitarajiwa kutumika kufikisha maji katika Miji mikubwa miwili ya Same na Mwanga kutoka Bwawa la Nyumba ya Mungu kilipo chanzo cha mradi huo.
Mkuu wa wilaya ya Same Kasilda Mgeni akiwa na kamati ya Usalama na viongozi wa chama cha Mapinduzi CCM kwenye wilaya hiyo wametembelea mradi kujionea maendeleo yake, ambapo kwa mujibu wa Msimamizi wa Mradi Mhandisi Emanuel Magembe mpaka sasa utekelezaji wake umefikia zaidi ya asilimia 70 upande wa wilaya ya Mwanga na zaidi ya asilimia 90 Upande wa Same.
“Kazi kubwa kukamilisha miundombinu ikiwemo mifumo ya Umeme katika eneo la Chanzo na Tangu serikali ilipohuwisha mkataba maendeleo ni mazuri na tunatarajia kukamilisha kazi hii hata kabla ya mwezi Julai ya makubaliano lakini wasiwasi uliopo ni kusuasua kwa upande mwingine kwa mkandarasi aliepewa kipande cha Same”. Alisema Mhandisi Emmanuel Magembe Mwakilishi wa Wizara ya Maji.
Aliseme mkandarasi huyo kwa sasa ameondoa baadhi ya mitambo kwa madai amecheleweshewa fedha zaidi ya shilingi Milioni 600 anazodai ambazo ni fedha za malipo ya kazi alizofanywa kwa awamu mbili kipindi cha kuanzia Januari – Juni mwaka 2023.
“Ni ukweli anadai na serikali haijamlipa lakini angetakiwa kuendelea na kazi kisha madai yake yanayochelewa yakaja na fidia kwakua ndio mkataba unavyo eleza, lakini pia kuna kiasi cha fedha Shilingi Milioni 900 ambazo kwa utaratibu anapewa mkandarasi kabla ya kuanza kazi tungetegemea angetumia fedha hizo wakati akisubiri fedha anazodai”.
Mkuu wa wilaya ya Same Kasilda Mgeni pamoja na kueleza masikitiko na wasiwasi wa kuchelewa kwa mradi, amewataka wakandarasi hasa wazawa wwanaoaminiwa na kupewa kazi na Serikali hasa kwenye miradi mikubwa kuwa wazalendo kwakua miradi hiyo inalenga kutoa huduma kwa wananchi.
“Bado ninaimani na serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassani na Waziri wa Maji Jumaa Aweso ninaamini changamoto hii itafuatiliwa kwa haraka ikiwezekana fedha ambazo imeonekana ndio kisingizio zitalipwa na mkandarasi atarudi eneo la kazi kukamilisha kazi iliyobaki mradi uweze kukamilika kwa wakati kama ilivyo ahidiwa kwa wananchi”. Alisema Kasilda Mgeni Mkuu wa Wilaya ya Same.
Mwakilishi wa Mkandarasi wa kampuni hiyo ya Agrivent Contraction Ltd. Mhandisi David Mbaga alisema kwa taarifa alizopewa na viongozi wake wa kampuni Mitambo iliyo ondolewa eneo la kazi ni kwaajili ya kufanyiwa Marekebisho (Services) ingawa suala la Madai lipo na kumekua na vikao vya mara kwa mara kufuatilia malipo ingawa bado hawajalipwa bado hawajafikia kuacha kazi.
Mradi mkubwa wa Maji Same, Mwanga-Korogwe Rasmi utekelezaji wake ulianza tangu mwaka 2014, ikipangwa hadi kukamilika kwake kuondoa kabisa changamoto ya upatikanaji wa maji katika Vijiji 38 , wilaya za Mwanga,Same na Korogwe, utekelezaji huo ukifanyika kwa awamu.