Msajili wa Vyama vya Siasa jaji Francis Mutungi akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua kikao kazi kati ya Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa na viongozi wa vyama vya siasa jijini Dar es Salaam.
Mkaguzi Mkuu wa Nje kutoka Ofisi ya CAG, Sylivester Kibona akifafanua baadhi ya mambo katika kikao kazi hicho kuhusu ukaguzi wa hesabu katika vyama vya siasa.
…………………………..
Na John Bukuku, Dar es Salaam
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini inatarajia kuanza kuhakiki vyama vya siasa vilivyopo kabla ya kuvisajili vyama vipya.
Mpaka sasa ofisi hiyo imepokea maombi ya vyama 18 ambavyo vinasubiri kupatiwa usajili wa muda.
Akizungumza leo Julai 17,2023 wakati wa kikao kazi na viongozi wa vyama vya siasa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amesema uhakiki huo utakaoanza Julai 20,2023 utafanyika Tanzania Bara na Zanzibar.
“Uhakiki uliokuwa nyuma ulikuwa wa vuta nikuvute, hatutaki hiyo hali tena, mnatakiwa mfahamu ninyi ni taasisi ambazo zinatakiwa zibebe sura njema ya taifa letu.
“Zoezi hili la uhakiki kama chama kimepoteza sifa kabisa za kuwa chama cha siasa tunakifutia usajili, tukishamaliza litaunganishwa na zoezi la usajili wa vyama vipya,” amesema Jaji Mutungi.
Amesema pia wamebaini kila mwaka kwenye ripoti za CAG hati chafu za vyama zinajirudia hivyo wameamua kulipa kipaumbele suala hilo ili kuvisaidia vyama kupata hati zinazoridhisha au hati safi.
Naye Naibu Katibu Mkuu Bara wa CCM, Anamringi Macha, amesema msajili amefanya vizuri kuandaa mafunzo hayo kwani yanalenga kuhakikisha vyama vinakidhi matakwa ya kisheria ya kuvianzisha.
Mwenyekiti wa Chama cha ADC, Hamad Rashid Mohamed, amesema mafunzo hayo ni muhimu na kuiomba Serikali iendelee kuyatoa kusaidia vyama ambavyo havina uwezo wa kusimamia ofisi.
“Bila kupata fursa ya mafunzo inawezekana kila wakati chama kikapata hati chafu. Vyama havina wahasibu wenye sifa, uchanga wa vyama na rasilimali ni tatizo kubwa,” amesema Mohamed.
Akiwasilisha mada kuhusu uandaaji wa taarifa za hesabu za vyama, Mkaguzi Mkuu wa Nje kutoka Ofisi ya CAG, Sylivester Kibona, amesema kila chama kinapaswa kuandaa na kuwasilisha taarifa zake kwa ajili ya ukaguzi.
“Tunatumia hekima kubwa sana kuwakagua, naomba muendelee kutupa ushirikiano hata pale panapotokea changamoto,” amesema Kibona.