Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso amefika, kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya Maji ya muda mfupi Wilaya ya Kasulu jimbo la Kasulu Mjini, akizungumza katika eneo la Mradi kata Kumunyika katika mradi wa Maji Mudandya na Mradi wa Maji Juhudi ikiwa ni sehemu ya ziara yake kata na maeneo mbalimbali Kasulu mjini ameonesha kutoridhishwa na kazi iliofanyika pamoja na matumizi ya fedha sambamba na kuchelewa kwa kukamilika kwa mradi.
Pia, Waziri Aweso ametekeleza agizo la Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango alilotoa tarehe 05 Julai 2023 kufika Kasulu mjini na kutatua changamoto kwa hatua za muda mfupi wakati Mradi mkubwa ukiendelea kutekelezwa.
Katika ziara yake, Waziri Aweso amesisitiza kazi kufanyika ndani ya miezi mitatu wananchi wapate maji kwa mikakati ya muda mfupi wakati Utekelezaji wa mradi mkubwa wa Maji Miji 28 Kasulu ukiendelea.
Aidha Waziri Aweso ametoa wito kwa wahandisi wa maji kuhakikisha wanatekeleza miradi kwa ufanisi na kwa wakati wakizingatia matumizi sahihi ya fedha.
Waziri Aweso ameweka wazi maelekezo ya kukaa pembeni kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Kasulu Mjini Eng Riziki Nyamtega na kuahidi kuleta uongozi mpya wilayani hapo na kuisuka upya Mamlaka hiyo ya Maji.
Akizungumza na wanachi ameahidi kuleta Milion 500 kuongeza nguvu katika kufanikisha miradi ya muda mfupi.
Katika kipindi cha Utekelezaji wa maagizo hayo Mhe Aweso ameelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Nzega Eng Athumani kilundumya kuisimamia Mamlaka hii katika kipindi cha Utekelezaji wa maagizo yake akiendelea kuiunda Mamlaka.
Waziri Aweso yupo mkoani Kigoma kufuatilia utendaji wa sekta ya Maji, kukagua Utekelezaji wa Miradi na utoaji huduma ya maji na uzinduzi wa Miradi iliokamilika akitarajia kupita Wilaya zote za mkoa wa Kigoma.