Na Mwandishi wetu, Simanjiro.
Katibu Hamasa na Chipukizi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Comrade Matei Damasi Siria ameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa namna inavyofanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo Wilayani Simanjiro.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Mazubu Grand Hotel, Mji mdogo wa Mirerani, Comrade Matei amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia imefanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo hivyo vijana wanampongeza.
Amesema kwenye Wilaya ya Simanjiro, Serikali ya awamu ya sita imefanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ya maji, elimu, afya, miundombinu ya barabara na mengineyo.
Amesema Tarafa za Emboreet na Terrat zimepata vituo vipya vya afya katika Kata za Loiborsiret, Terrat na Komolo, hivyo kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
Amesema Rais Samia kupitia fedha za UVIKO-19 ameweza kujenga madarasa kwenye kila sekondari hivyo kuwaondolea adha wananchi wa hali ya chini kuchangia madawati au madarasa ili watoto wao waweze kuanza kidato cha kwanza na darasa la kwanza.
“Tumeona miradi mbalimbali ya maji kwenye maeneo tofauti ya Simanjiro ikiwemo mradi mkubwa wa mto Ruvu kutoka Kata ya Ruvu Remit hadi mji mdogo wa Orkesumetu na pia kata mbalimbali zimenufaika na RUWASA maji bombani ikiwemo kata za Loiborsiret, Terra, Naberera na mji mdogo wa Mirerani, hivyo tunamshukuru Rais Samia, kwa namna ambavyo wananchi wananufaika,” amesema Comrade Matei.
Amesema madarasa ya shule ya msingi, sekondari yamejengwa ikiwemo shule ya awali na msingi ya Bilionea Saniniu Laizer iliyopatiwa fedha kupitia mradi wa BOOST.
“Hivi karibuni jijini Dodoma kwenye Bunge la Bajeti la mwaka 2023/2024 tumeona namna ilivyopitishwa barabara ya lami kutoka Arusha inayopitia kwetu Simanjiro kupitia Oljoro namba tano, Komolo, Terrat, Naberera, Orkesumet, kwenda Kiteto hadi Kongwa Mkoani Dodoma,” amesema Comrade Matei.
Amesema katika kuwajengea uwezo vijana nchini kupitia kilimo, pia vijana wa Simanjiro hawakupishwa na mradi huo kwani waliweza kuchaguliwa na kushiriki kujengewa uwezo na Wizara ya Kilimo.
Amesema wao kama vijana wa Simanjiro, watamlinda na kumsemea mema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, ili aweze kuwatumikia na kuwaletea maendeleo wananchi wake na hawapo tayari kukaa kimya kwa mtu yeyote atakayemsema vibaya au kupinga juhudi thabiti za maendeleo.
“Tutasimama kidete na Mama yetu Rais Samia, mahali popote katika kumpongeza kwa namna anavyomwaga miradi ya maendeleo hapa kwetu Simanjiro, kama maji yanavyotiririka kwenye kina kirefu,” amesema Comrade Matei na kuongeza;
“Sisi kama vijana hatupo tayari kuona mtu awaye yeyote akimyumbisha mama kwani Rais Dkt Samia akiyumbishwa hata nchi itayumba hivyo tutasimama kidete kumuunga mkono na kumtetea Rais wetu.”
Hata hivyo, ameupongeza uongozi wa Wilaya ya Simanjiro kuanzia DC Dkt Suleiman Hassan Serera, Mwenyekiti wa CCM Kiria Ormemei Laizer, Mbunge wa Jimbo Christopher Ole Sendeka, Mwenyekiti wa Halmashauri Baraka Kanunga, DED Simanjiro Gracian Max Makota, Madiwani na watumishi wote, kwa namna wanavyosimamia na kufanikisha maendeleo ya eneo hilo.