*********************************
(Jovina Bujulu, MAELEZO, Dar es salaam)
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli
imefanikiwa kutimiza ahadi zilizoahidiwa kwa wananchi wakati wa kampeni za
Urais, mwaka 2015, na wakati wa ufunguzi wa Bunge la 11 la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Novemba 2015.
Rais alihutubia Bunge kwa mujibu wa matakwa ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 91, ibara ndogo ya kwanza inayomtaka Rais aliyechaguliwa kufungua rasmi Bunge hilo.
Akihutubia bunge hilo, Rais Magufuli aliwaambia wabunge kuwa wananchi
waliwachagua wakiwa na matarajio makubwa na watawapima kwa namna
watakavyokidhi kiu na matarajio yao.
“Wananchi wamewapa imani na ridhaa ya kuwawakilisha katika kipindi cha Awamu ya Tano ambapo matarajio yao ni makubwa sana, sote tuliahidi kuwatumikia na kutokana na utumishi wetu kwao tuweze kutatua matatizo yao mbalimbali na kuongoza mabadiliko makubwa ya kiutendaji” alisema Rais Magufuli.
“Mimi na Mhe. Samia, Makamu wa Rais tuliwaahidi wananchi kuwa tutawatumikia na kuhakikisha kuwa katika utumishi wetu tutawajali wananchi wote, lakini zaidi wananchi wa kawaida” alisema Rais Magufuli.
Ni dhahiri uchapakazi wake umeonyesha mabadiliko makubwa ya kiutendaji,
tumeshuhudia Rais akifanya mikutano mbali mbali na viongozi kuanzia ngazi ya
mawaziri hadi watendaji wa kata Tanzania bara na kuzungumza nao masuala
mbalimbali ya kiuongozi ikiwemo wajibu wao kwa wananchi.
Mkutano kati ya Rais na watendaji wa kata ni mwendelezo wa mikutano yake na
watendaji wa serikali wakiwemo Wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa,
Wakuu wa wilaya, Wakurugenzi wa wilaya, Makatibu tawala ya wilaya na Makatibu
watendaji wa tarafa.
Akizungumza na Makatibu watendaji wa tarada Rais alisema “Ninyi ni wawakilishi
wangu ngazi ya kata, tunapozungumza mafanikio ya Serikali, ninyi ndio wasimamizi
wa mwanzo wa mafanikio hayo.”
Hatua ya Rais kuwaita Watendaji hao wa tarafa kutoka Tanzania Bara na
kuzungumza nao, ni kitendo kinachoonyesha jinsi anavyowajali viongozi wote
kuanzia ngazi ya chini hadi juu. Pia ni kitendo kinachoonyesha kuwa uongozi wa
chini ukifanya kazi vizuri utawezesha hata uongozi wa juu kutenda kazi kwa ufanisi
na yenje tija kwa taifa na wananchi kwa ujumla.
Katika bunge hilo Rais pia aliahidi kusimamia matumizi ya mali za umma na
rasilimali za Taifa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa rasilimali zetu zinatumika
kwa matumizi kwa manufaa ya umma na si kwa manufaa ya mtu binafsi. Aidha,
kuhakikisha kuwa ugawaji wa rasilimali hizo unafanyika kwa haki.
Katika siku za mwanzo za utawala wake Rais Magufuli alianza kwa kufanya
ufuatiliaji wa rasilimali zetu ambapo aliunda kamati maalum ya kuchunguza mchanga na madini yalikuwa yanasafirishwa nje ya nchi. Kamati hiyo ilionyesha
upotevu mkubwa wa mapato na rasilimali za nchi ambapo nchi ilikuwa inapoteza
kiasi cha bilioni 829.4 hadi trilioni 1.439 kwa kusafirisha mchanga nje ya nchi.
Ili kuhakikisha anazuia upotevu huo, kamati ilitoa mapendekezo kadhaa ambayo
Rais aliyakubali. Miongoni mwa mapendekezo hayo ni usitishwaji wa usafirishaji
wa mchanga huo hadi mrabaha stahiki utakapolipwa, na kujengwa kwa vinu vya
kuchakata madini yote ili yaweze kufahamika na kutozwa kodi.
Aidha, Rais aliwaagiza Wakuu wa mikoa inayozalisha madini kuanzisha masoko ya
madini ili kudhibiti utoroshaji na uuzaji holela wa madini. Hadi sasa baadhi ya
masoko yamekwisha anzishwa katika mikoa ya Mwanza, Geita, Dar es salaam,
Mtwara, Manyara, Morogoro, Kagera na Arusha. Kwa upande wa wilaya masoko
hayo yamefunguliwa Simanjiro na Chunya.
Ufunguzi wa masoko hayo umeleta neema si kwa Serikali tu bali hata kwa wauzaji wa madini hayo ambao walikuwa wakiyauza kwa kudhulumiwa na wanunuzi wakubwa. Kwa Serikali na nchi kwa ujumla masoko haya yameongeza pato la taifa kwa kiasi kikubwa na ongezeko la upatikanaji wa madini.
Eneo lingine ambalo Rais aliahidi kulishughulikia ni kusimamia ukusanyaji wa
mapato na matumizi mabaya ya fedha za umma. Katika kutimiza ahadi yake kwa
upande wa kusimamia mapato tumeshuhudia Rais akifanya mabadiliko ya mara kwa mara ya uongozi katika mamlaka ya kukusanya kodi (TRA) na kuzindua kituo kikuu cha Taifa cha kuhifadhi mifumo ya ukusanyaji wa mapato kwa njia ya elektroniki ambapo makusanyo ya mwezi Septemba 2019 yalikuwa trilioni 1.7 sawa na asilimia 97.20 kiasi ambacho ni hakijawahi kukusanywa na mamlaka hiyo tangu kuanzishwa kwake Julai mosi, 1996.
Ni dhamira ya TRA kukusanya mapato kwa utaratibu rahisi na wa wazi na
walipakodi watapata urahisi wa kupata huduma zinazotolewa kwa wakati.
Matokeo ya kuongezeka kwa ukubalifu yatadhihirika kwa kuongezeka kwa mapato kwa ajili ya Serikali kutoa huduma za jamii zinasostahiki na kwa ubora. Hii itaifanya jamii ya walipakodi kufurahia manufaa ya kijamii na kiuchumi kutokana na kodi wanazolipa katika kuboresha hali ya maisha.
Kituo hiki ni mashirikiano ya pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), ambacho kimeundwa ili kusaidia kuondoa mianya ya uvujaji wa mapato ya serikali zote mbili.
Akizindua kituo hicho Rais alizitaka taasisi mbalimbali zikiwemo za Serikali,
kampuni na benki kujisajili katika kituo hicho ili kuweza kukusanya kodi kwa
ufanisi. ‘Kituo hicho ni muhimu sana kwa ustawi wa maendeleo ya nchi ili kulinda
usalama wa taifa, taasisi za serikali na makampuni binafsi yanayoendesha shughuli
zake nchini na kukuza sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano ambayo ni
kichocheo kikubwa cha maendeleo’ alisema Rais.
Katika kuhakikisha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inakuwa kinara wa utawala
bora, Rais aliahidi kupambana na rushwa na ufisadi. Awali akihutubia bunge la
kwanza, Rais aliwaambia wabunge kuwa mojawapo ya maeneo yaliyolalamikiwa na
wananchi wakati wa kipindi cha kampeni ni rushwa ambapo sehemu nyingi wananchi walisema kuwa rushwa ni mojawapo ya kero kubwa wanazokumbana
nazo.
Baadhi ya mafanikio ya mapambano ya vita dhidi ya rushwa ni pamoja na
kuanzishwa kwa ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
Hadi ngazi za wilaya. Pia Serikali hii inajipambanua kwa uwazi na uwajibikaji
katika utoaji wa huduma kwa umma, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa utoaji wa
elimu kwa umma kuhusu rushwa na madhara yake.
Katika mkutano wa 32 wa wakuu wa nchi za Afrika (AU) uliofanyika Addis Ababa,
Ethiopia mwaka 2017, Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alisema
kuwa Tanzania ilitajwa kuwa miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika
ufuatiliaji na utekelezaji wa mapambano dhidi ya rushwa.
Taasisi ya Transparency International imesifu juhudi za Rais Dkt. John Pombe
Magufuli na kuitaja Tanzania kuwa ni nchi ya pili kwa kupunguza rushwa na
kufanikiwa kuifanyia kazi mianya mingi ya rushwa.
Akizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam aliyekuwa Mkurugenzi wa
TAKUKURU, CP. Diwani Athuman alisema kuwa utafiti uliofanywa na taasisi za
kimataifa za Transparency International na Afro Barometer inayoitwa Global
Corruption Barometer Africa 2019, alisema kuwa Tanzania ni ya kwanza kati ya
nchi 35 za Afrika katika kipengele cha juhudi za serikali katika kupambana na
rushwa kwa mwaka 2019.
Aliongeza kusema kuwa Tanzania imefanya vizuri katika maeneo mawili ambayo ni utendaji mzuri wa Serikali na kukuza imani kwa wananchi dhidi ya Serikali yao na jitihada za kupambana na rushwa.
Kuhusu kero ya migogoro ya ardhi, Serikali ya Awamu ya Tano imefuta mapori
tengefu 12 yenye ukubwa wa ekeri 707,659.94 ambayo yamepoteza sifa na
kuyagawa kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za makazi, kilimo na ufugaji, na
misitu 7 yenye ukubwa wa ekari 46,715 kurudi kwa wananchi.
Hatua hii ilifuatiwa na kubaini uwepo wa vijiji 975 vyenye migogoro, ambapo
iliamuliwa kuwa vijiji 920 vibaki ndani ya hifadhi na mipaka irejerewe upya na
kupatiwa vibali vya ardhi vya kijiji. Pia serikali iliridhia kumega misitu 14 kwa ajili ya kilimo na mifugo na kufuta mashamba 16 yasiyoendelezwa ili yapangiwe
matumizi ya kilimo na mifugo.
Ahadi nyingine ambazo Rais amezitimiza ni katika sekta ya afya na elimu ambapo katika elimu aliahidi elimu bure kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne.
Kutokana na utekelezaji wa ahadi hiyo, kumekuwa na mwamko mkubwa wa wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao shule ambapo kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaoandikishwa darasa la kwanza shule ya msingi ambao idadi yao imefikia 1,670,919 mwaka 2019 kutoka 896,584 mwaka 2016. Kwa upande wa shule za sekondari idadi ya wanafunzi walioandikishwa kwa mwaka 2019 ni 710,436 kutoka wanafunzi 238,365 walioandikishwa mwaka 2016 wakati sera ya elimu bure ilipoanza kutekelezwa nchini.
Katika sekta ya elimu pia tumeshuhudia maboresho mbalimbali ambapo vifaa vya kufundishia na kujifunzia vimeongezwa, michango isiyo ya lazima imeondolewa, kuongezewa madawati na kujengwa kwa nyumba za walimu.
Aidha, katika eneo la afya, dhamira ya Rais kujenga uchumi wa kisasa na suala la kupambana na umaskini amelipa msukumo wenye tija ili kuwa na wananchi wenye afya bora. Tumeshuhudia uboreshaji wa sekta hii ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za afya, kuzipatia vifaa bora na vya kisasa hospitali, vituo vya afya na zahanati. Lengo likiwa ni kuwaondolea usumbufu wananchi na kutolazimika kupeleka watu kutibiwa nje ya nchi.
Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Awamu ya Tano, Kwa tumeshuhudia mafanikio mengi katika sekta mbalimbali kama vile sekta za afya, elimu, miundombinu, nishati na madini, ikiwa ni kutimiza ahadi ambazo ziliahidiwa na Rais wakati anaingia madarakani. Maendeleo yote haya yamewagusa wananchi kwa kiasi kikubwa kwa sababu yameweza kutatua kero nyingi ambazo wananchi walikuwa nazo.