Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Nchechu akizungumza leo tarehe 13/7/2023 Jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Wahariri wa Vyombo vya habari uliofanyika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere.
Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Frank Nyabudenge akifafanua jambo katika kikao kazi kati na Wahariri wa Vyombo vya habari uliofanyika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere.
Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Bw.Nevelle Meena akizungumza jambo katika kikao kazi kati Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Wahariri wa Vyombo vya habari uliofanyika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere.
Mhariri na Mkurugenzi Mkuu wa Full Shangwe Blog & Tv John Bukuku akichangia mada katika kikao kazi kati Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Wahariri wa Vyombo vya habari uliofanyika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere.
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Nchechu amezitaka Taasisi na Mashirika ya Umma kutekeleza majukumu kwa ufanisi kwa kuzingatia maslahi ya Taifa ili kuleta tija kwa jamii.
Akizungumza leo tarehe 13/7/2023 Jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Wahariri wa Vyombo vya habari uliofanyika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere, Bw. Mchechu, amesema kuwa
taasisi za umma zinapaswa kueleza kwa jamii mazuri ambayo wanafanya ili waweze kujua na kupata fursa ya kushauri.
Bw. Mchechu amesema kuwa Benki ya TADB imepata nafasi ya kuongeza na wahariri pamoja na waandishi wa habari na kueleza mambo mbalimbali yanayofanyika katika kutoa huduma kama ilivyokusudiwa.
“Imeongezeka ushirikishwaji wa taasisi na mashirika pamoja na kufanya mabadiliko ya kiutendaji kupitia maoni ya wadau mbalimbali” amesema Bw. Mchechu.
Amefafanua kuwa lengo ni kuhakikisha kunakuwa na mawasiliano makubwa ya mashirika na wahariri wa vyombo vya habari ili watanzania waweze kujua yanafanya nini.
Hata hivyo ameitaka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuwa na mikopo nafuu ili kuwapata walengwa kwa urahisi pamoja na kuendelea kutoa elimu juu.
“Mazao yanachukua muda mrefu kuvuna unapomuambia mkulima atalipa mkopo baada ya muda mfupi anawaza kuwa bado hajavuna” amesema Bw. Mchechu.
Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Frank Nyabudenge, amesema kuwa lengo ni kuhakikisha wanatoa mitaji katika sekta ya kilimo kwa kuongeza kasi ya utoaji wa mikopo kwa wakulima.
Bw. Nyabudenge amesema kuwa idadi utoaji wa mikopo imekuwa ikipanda kwani walikuwa na mikopo ya shilingi bilioni 110 na kupanda hadi kufikia shilingi bilioni 152.
Amesema kuwa pia imetoka shilingi bilioni 262 na hadi kufikia Juni 30, 2023 tulikuwa na jumla ya mikopo Shillingi bilioni 317.
“Tunaamini hadi kufikia mwezi Desemba mwaka huu utoaji wa mikopo itaongezeka, lengo ni kutanua wigo wa benki pamoja na kubadili mfumo wa kilimo Tanzania, lakini pia kuchagiza taasisi nyingine za kifedha kutoa mitaji kwa wakulima ”amesema Bw. Nyabudenge.
Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Bw.Nevelle Meena, amesema kuwa ni vizuri taasisi na mashirika ya umma wakatoa ushirikiano kwa vyombo vya habari ili kuweza kufikia malengo tarajiwa.
Amesema kuwa TEF wapo katika mpango wa kukutana na mashirika yote ya umma ili kujua wanafanya nini katika kutekeleza majukumu na kufikisha taarifa kwa umma.
“Baadhi ya taasisi wametengeneza mazingira kwa kujiweka mbali na vyombo vya habari jambo ambalo sio rafiki kutokana umma wanashindwa kujua nini kinaendelea” amesema Bw. Meena.