Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete
Na Mwamvua Mwinyi, Kisarawe
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete amemuagiza ofisa Utumishi wilaya ya Kisarawe Baptista Kihanza kuondoa kilio vya watumishi wanaotakiwa kupandishwa madaraja ndani ya mwaka huu wa fedha.
Aidha amemtaka apeleke taarifa za mwanzo za utekelezaji za utekelezaji wa agizo hilo, Ofisini kwake ndani ya wiki tatu zijazo,zinazoeleza aidha mchakato huo kaunza ama umemalizika.
Akizungumza na watumishi na wakuu wa idara mbalimbali Kisarawe, Ridhiwani alieleza, anahitaji utekelezaji ufanyike haraka,hataki kusikia lugha yeyote nyingine.
Vilevile ameelekeza changamoto ya kushushwa mishahara kwa watumishi ambao wamekwenda kujiendeleza kimasomo ili kupandishwa madaraja lakini wameshushwa mishahara yao badala ya kupandishwa , changamoto hiyo nayo itatuliwe.
Kuhusu changamoto ya kukithiri Ukaimu kwa kipindi kirefu kwenye Idara mbalimbali wilayani Kisarawe, Ridhiwani alieleza amelibeba tatizo hilo na atalifanyia kazi.
“Unakuta mtumishi anakaimu idara ,Tena bila sifa kwa miezi zaidi ya sita ,mnaweza kuona kama mzaha lakini mnapokaimu kaimu idara hizi ,kuna haki mnazikosa, waangaliwe watumishi wenye sifa kwenye idara hizo ,na sio kuweka watu ambao hawana sifa za kukaimu idara hizi”alifafanua Ridhiwani.
Ridhiwani alieleza kwamba, barua ya kukaimu inatoka kwa Katibu Mkuu wa wizara kabla ya kukaimishwa Katibu Mkuu anatakiwa apate sifa zako.
“Kukaimu kiutaratibu mwisho miezi sita, ofisa Utumishi wilaya andika barua kwa Katibu Mkuu kumkumbusha Kuwa una uhitaji mkubwa wa wakuu wa idara katika wilaya yako ili usaidiwe.”alisema Ridhiwani.
Pamoja na hayo, aliwataka maofisa Utumishi nchini kufanya kazi kwa ubunifu, na kutatua kero za watumishi ili kuboresha utendaji kazi.
“Nataka kusikia kila Ofisa Utumishi anajiwekea ratiba ya kuzungumza na watumishi anaowasimamia ili kusikiliza maoni, malalamiko au changamoto zozote wanazokutana nazo kwa lengo la kuboresha utumishi wa umma nchini .
” Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka Maofisa Utumishi kuwa wasemaji wa watumishi wanaowasimamia,Kuwa wabunifu na kutatua kero na changamoto za watumishi.”
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Baptista Kihanza ambae pia ni ofisa Utumishi wilaya aliahidi kwenda kuyafanyia kazi maagizo yote.
Licha ya hayo, alieleza wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vyombo vya usafiri ,vitendea kazi, ukosefu wa motisha kutokana na ufinyu wa bajeti pamoja na uhaba wa watumishi ,kwani mahitaji 3,272 na waliopo ni 2,033