***************************
NA EMMANUEL MBATILO
Chama cha Mapinduzi CCM kimesema kinaunga mkono nchi zingine ambazo zinataka kuondolewa kwa vikwazo mbalimbali kwa nchi ya Zimbabwe, ili wananchi wake waweze kufanya maendeleo bila masharti yeyote.
Hayo yamesemwa leo na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bw.Philip Mangula katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ndogo ya Chama cha Mapinduzi Lumumba.
Akizungumza katika mkutano huo Bw.Mangula amesema kuwa CCM kinaamini vikwazo dhidi ya Zimbabwe ni mwendelezo wa fikra na matendo ya uonevu na unyanyasaji kwa Waafrika.
“Zimbabwe inapaswa kupiga hatua za haraka za maendeleo, uchumi na kijamii kwa watu wake”. Amesema Bw.Mangula.
Hata hivyo CCM imetoa kauli hiyo kipindi ambacho Marekani imemwekea vikwazo balozi wa Zimbabwe nchini Tanzania, Anselem Sanyatwe kwa tuhuma za kuwaamuru wanajeshi wa nchi hiyo kuwafyatulia risasi za moto waandamanaji waliokuwa wakipinga kitendo cha Tume ya uchaguzi Zimbabwe kuchelewa kutangaza matokeo.