Home Mchanganyiko NCHI ZA AFRIKA ZATAKIWA KUWAJENGEA UWEZO WATAALAM WA JIOLOJIA

NCHI ZA AFRIKA ZATAKIWA KUWAJENGEA UWEZO WATAALAM WA JIOLOJIA

0

Wataalam wa Jiolojia kutoka nchi mbalimbali wakifuatilia ufunguzi wa
Mkutano wa 36 wa Wataalam wa Jiolojia.

Waziri wa Madini Doto Biteko akifungua Mkutano wa 36 wa Watalaam wa
Jiolojia kutoka nchi mbalimbali za Afrika.

**************************************

Na Asteria Muhozya, DSM

Waziri wa Madini Doto Biteko ametoa wito kwa kuzitaka nchi za Afrika
kujenga uwezo kwa Wataalam wa ndani wa Jiolojia ili kuwawezesha
kujenga uwezo wa tafiti za rasilimali madini ili pindi nchi au taasisi wafadhili
wanapoacha kufadhili, mamlaka husika ziwe kwenye nafasi ya kuendeleza
shughuli hizo.

Waziri Biteko ameyasema hayo Oktoba 24, 2019 wakati akifungua
Mkutano wa 36 wa Wataalam wa Jiolojia kutoka nchi mbalimbali za Afrika
ambao wanakutana jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo unalenga katika kuwapatia wataalam hao mafunzo
yanayogusa masuala mabalimbali kuhusu sekta ya Madini ikiwemo
kubadilishana uzoefu katika utafutaji rasilimali madini na kuangalia namna
bora ya kuendeleza rasilimali hizo ili kuhakikisha kwamba zinayanufaisha
mataifa husika.

Aidha, amewataka washiriki wa mkutano huo kujifunza na kutumia vyema
uzoefu mzuri utakaotolewa na mataifa mengine ili kuwezesha kuongeza
thamani katika kutekeleza majukumu ya taasisi zao katika uendelezaji wa
rasilimali madini.

‘’ Afrika lazima tujifunze wenyewe kuendeleza na kujenga miradi yetu
wenyewe. Katika mkutano yapasa kujiuliza siku Wafadhili wetu Umoja wa
Ulaya na taasisi nyingine zinazofadhili mafunzo haya zikiacha tutaweza
kujisimamia wenyewe?,’’ amehoji Waziri Biteko.

Amesema kwa upande wa Tanzania kama taifa linaamini katika
kuwajengea uwezo wataalam wa ndani ambapo tayari serikali imechukua
hatua kadhaa za kuhakikisha zinawendeleza wataalam wake ili kuwezesha
taifa kuzalisha wataalam waliobobea katika taaluma ya jiolojia na ambao
watakuwa na mchango katika utafutaji wa rasilimali madini.

Amesema mradi huo wa kutoa Mafunzo kwa Taasisi za Jiolojia Afrika
unafadiliwa na Umoja wa Ulaya pamoja na taasisi nyingine 12 ambapo
tangu kuanzishwa kwa mradi huo mnamo mwaka 2017, tayari
umewezesha kuwapatia mafunzo wataalam wapatao 1,100 kutoka Mataifa
mbalimbali ya Afrika huku wataalam 30 wa Tanzania wakiwa wamepatiwa
mafunzo hayo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkuu wa Idara ya Ushirikiano Kutoka Umoja
wa Ulaya, Jose Dorreia Nunes, amewataka washiriki wa mkutano huo
kutafakari namna rasimali hizo zitakavyozinufaisha nchi zao ikizingatiwa
kwamba madini ni chanzo kikubwa cha mapato kwa nchi za Afrika hivyo ni
muda sahihi kupitia mafunzo yanayotolewa na Umoja huo yawezeshe
kujenga uwezo wa wataalam wa ndani katika kutafiti, kusimamia na
kuendeleza rasilimali katika nchi zao.

Naye, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini
Tanzania (GST), Yorkberth Myumbilwa akizungumza na waandishi wa
habari waliohudhuria mkutano huo amesema mafunzo yanayotolewa na
Taasisi wafadhili yana umuhimu mkubwa kwa kuwa yanagusa moja kwa
moja shughuli zinazofanywa na taasisi hizo zikiwemo tafiti, wingi wa
mashapo, urithi wa Jiolojia, namna ya kuhifadhi data na masuala mengine.

Ameongeza kwamba, suala la kukutanishwa na taasisi nyingine lina
umuhimu kwa GST kwa kuwa linawezesha kujenga mahusiano mapya na
Taasisi nyingine za Jiolojia kutoka nchi nyingine.

Nchi zinazoshiriki mkutano unafanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 24 –
25 Oktoba, 2019 ni pamoja na Tanzania, Namibia, Sengel Morroco, Kenya,
Afrika Kusini , Rwanda, Zambia na Ghana.