Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo amepongeza ushirikiano na uhusiano mkubwa uliopo baina ya Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watendaji wa Halmashauri kisiwani Pemba hatua iliyowezesha utekelezaji na uwekezaji mkubwa wa miradi ya maendeleo kwa wananchi.
Akifungua mafunzo ya usimamizi wa fedha mfuko wa kuchochea maendeleo ya Jimbo kwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliopo na Watendaji Halmashauri za Wilaya na Mabaraza ya Mji kisiwani Pemba Julai 12, 2023, Waziri Jafo ameelezea kufurahishwa kwake na mshikamano huo ambao umeongeza kasi ya kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Waziri Jafo amesema Wabunge wote wa Zanzibar kutoka Ungujana Pemba kupitia vikao na kamati za Bunge wamekuwa na mchango mkubwa wa kusemea vipaumbele vya miradi ya maendeleo iliyopo katika majimbo yaoambapo juhudi zimewezesha Serikali ya Mapinduzi ya Mapinduzi Zanzibar kupokea kiasi kikubwa cha fedha za miradi ikiwemo ikiwemo Shilingi Bilioni 230 ambazo fedha za miradi ya UVIKO 19 zilizotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Jana nikiwa Unguja nilipata fursa ya kutembelea miradi ya fedha za UVIKO 19 na sote ni mashahidi tulishudia manufaa ya fedha hizi ambazo ni nyingi sana kuzipata kwa mkupuo mmoja katika kutekeleza miradi ya maendeleo inayogusa wananchi na mfano mzuri ni mradi wa maji uliotengewa kiasi cha Shilingi Bilioni 34 utakaotekelezwa kwa wananchi wa Unguja na Pemba” amesema Waziri Jafo.
Akifafanua zaidi Waziri Jafo amesema mafanikio hayo ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo yanatokana na mshikamano wa Wabunge wa Zanzibar katika kufuatilia kwa karibu mijadala inayoendelea ndani ya Bunge la Jamhuri ya Tanzania na kuonesha wajibu na nafasi zao katika chombo hicho cha uwakilishi.
Aidha Dkt. Jafo amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Mwinyi kwa juhudi na mshikamano mkubwa katika dhamira ya waliyonayo katika kuhakikisha Zanzibar inapiga hatua kubwa ya maendeleo kupitia miradi mikubwa ya uwekezaji ambapo katika kipindi cha miaka miwili ya Uongozi wao mafanikio makubwa yamepatikana.
Akitolea mfano Waziri Jafo amesema ndani ya Kipindi cha miaka miwili ya Viongozi hao, takribani Dola za Marekani Milioni 400 tayari zimepatikana kwa ajili ya kuteleza mradi wa Beatification of Zanzibar ambao unalenga kuimarisha miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Pemba.
“Hizi ni fedha zinazotoka moja kwa moja Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na zinakuja kutekeleza mradi wa BZ (Beatification of Zanzibar) na tayari tumeona utekelezaji wake barabara ya makunduchi-Tunguu, Unguja na Pemba mradi wa Uwanja wa Ndege na barabara ya Mkoani kwenda Wete. Hizi zote ni juhudi za Wabunge katika hawa kusemea miradi ndani ya Bunge” amesema Dkt. Jafo.
Amesema ipo miradi mingine mikubwa ya kimakati inayoendelea kutekelezwa Zanzibar ikiwemo mradi wa umeme wa ZESTA wenye thamani ya Dola Milioni 100 ambapo Zaidi ya Megawati 30 zitatokana na umeme wa jua na kufanya miradi hiyo kuwa na manufaa endelevu kwa jamii na wananchi wa Unguja na Pemba.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Dkt. Idrisa Muslih Hijja ameishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kwa kuitisha mafunzo hayo kwa wabunge wa Unguja na Pemba kwa kuwa yatasaidia kujenga uelewa wa pamoja wajibu na majukumu ya Wabunge na Watendaji katika kusimamia mfuko wa maendeleo ya jimbo.
Ameongeza kuwa Ofisi yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais itahakikisha inakusanya na kuchakata maoni, ushauri na mapendekezo yote yatakayotolewa na kuyawasilisha katika mamlaka zinazohusika kwa ajili ya utekelezaji wa masuala ya kisera na kisheria.
Idrisa amesema Serikali itaendelea kuweka mifumo ya uwazi na uwajibikaji katika mifumo hiyo ili kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha za mfuko wa jimbo ambao unakusudia kutekeleza miradi ya huduma za kijamii na kiuchumi inayoibuliwa na wananchi katika majimbo ya uchaguzi.
Akitoa salamu za shukrani kwa Wabunge hao, Mbunge wa Chambani, Mkoa wa Kusini Pemba, Mhe. Mohamed Abdulrahman Mwinyi, amemshukuru Waziri Jafo kwa kuwezesha Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka Pemba kupata mafunzo hayo ambayo yalikuwa ni kilio chao cha muda mrefu kupata uelewa kuhusu wajibu na nafasi ya wabunge katika usimamizi wa fedha za mfuko wa maendeleo ya Jimbo.
Akiwasilisha mada kuhusu Sheria ya Mfuko wa Jimbo, Wakili Mkuu wa Serikali kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Wankyo Mkono amesema Sheria hiyo iliwekwa makhususi kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia uratibu wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira na Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Ameongeza kuwa fedha za miradi hiyo hutengwa katika Bejeti kuu ya Serikali ambapo asilimia 25 ya fedha hizo zinagawanywa sawa katika kila jimbo na asilimia 75 inawaganywa kulingana na idadi ya watu katika jimbo, hali ya umaskini na ukubwa wa Jimbo husika na Mbunge wa Jimbo husika ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya mfuko huo.
Kwa mujibu wa sheria fedha hizi ni kwa ajili ya kuchochea miradi ya maendeleo ya wananchi katika majimbo na sheria imeenda mbali zaidi kwa kutoa katazo kwa fedha hizi kutolewa kama zawadi na masuala ya kisiasa” amesema Wankyo.