Na. Majid Abdulkarium, Mbozi -Songwe
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt Grace Magembe amewataka watumishi wa Afya nchini kuacha kufanya kazi kwa mazoea bali kufuata taratibu za kazi kwa kuzingatia maadili, weledi na viapo vya taaluma zao, jambo ambalo Mhe Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesikika akilisistizia mara kadhaa.
Dkt. Magembe ametoa wito huo leo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea Kituo cha Afya cha Isansa, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe na Hospitali ya Wilaya ya Mbozi –Vwawa Mkoani humo
Dkt. Magembe amesema kuwa ni wajibu wa kila mtumishi kuzingatia maadili ya taaluma yake na kufanya kazi kwa weledi ili kutoa huduma bora kwa watanzania.
“Sisi wateja wetu ni wananchi wanaokuja kupata huduma, hivyo tuboreshe mawasiliano na wateja wetu, tutumie lugha za staha, tuwahudumie kwa wakati, kama mnakuwa na dharura au kitu kingine, mnawajibika kuwapa taarifa sahihi wagonjwa na ndugu wanaosubiri wagonjwa na sio kuwaacha wamekaa kwenye mabenchi bila taarifa yoyote” amesisitiza Dkt. Magembe
Pia, ameelekeza Mganga mkuu wa Mkoa kwa kushirikiana na Timu ya Afya ya Mkoa kufanyika ukaguzi wa mara kwa mara wa bidhaa za dawa, vifaa tiba na huduma zinazotolewa katika vituo vya kutolea huduma ili kuleta ufanisi, kupata takwimu sahihi za mahitaji katika kituo husika na kudhibiti matumizi mabaya ya bidhaa za afya.
“Tumefanya ukaguzi wa baadhi ya bidhaa za afya hapa Vwawa na umeona mapungufu yaliyojitokeza, kwa kuwa niko hapa na Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI, tutalitolea kauli hili katika ziara hii”
Dkt. Magembe ameeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa pesa nyingi katika kuboresha sekta ya afya nchini hivyo ni wajibu wa wataalamu wa afya nchini kutoa huduma bora kwa wananchi.
Aidha, amewapongeza watumishi wa Afya wanaofanya kazi vizuri na hata wananchi wamekuwa wakiwataja katika matukio mbalimbali, amewataka Waganga wafawidhi wa vituo vya afya na hospitali nchini kufanya vikao na watumishi wao ili kujua mahitaji na changamoto mbalimbali walizonazo na kuzifanyia kazi kwa lengo la kuwaboreshea mazingira yao ya kazi na kuleta matokeo chanya ya utoaji huduma bora.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Dkt. Charles Mahera amewataka watumishi hao kuboresha utendaji kazi utakaoendana na thamani ya uwekezaji uliofanyika katika vituo vya kutolea Huduma za afya.
Dkt. Mahera ameweka wazi kuwa lengo la ziara hiyo ni kuangalia maendeleo ya miradi ikiwemo ya Global Fund, utolewaji wa huduma, uzingatiaji wa miongozo na matumizi ya rasilimali za afya ikiwemo watumishi, fedha, miundombinu, dawa na bidhaa za afya kwa lengo la kuwaboreshea wananchi huduma.
“Tufanye kazi kwa bidii kwani serikali ipo pamoja na nyinyi katika kuboresha maslahi yenu na kuongeza watumishi ili wananchi wapate huduma sahihi na kwa wakati”, ametoa wito Dkt. Mahera
Naye, Mkuu wa Programu kutoka Wizara ya Afya Dkt.Catherine Joachim, amesisitiza watumishi hao kutumia mifumo kwa ufasaha ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi na kwa kufanya hivyo itasaidia kusimamia mapato ya vituo vyao.