Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako akimkabidhi Dada Mkuu wa shule ya sekondari Jikomboe Vaertina Geofrey kiasi cha shilingi 500,000 kwa ajili ya kuwezesha kupika pilau na kuku kwa muda wa siku tatu baada ya kufurahishwa na ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha sita wa shule hiyo ambao walipata daraja la kwanza na la pili tu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akishiriki katika ujenzi wa Ofisi za Uthibiti ubora wa Shule wilayani Chato alipofika kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi hiyo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako akikagua ujenzi wa bwalo la chakula katika shule ya sekondari Jiomboe wakati akiwa katika ziara ya kikazi Halmashauri ya wilaya ya Chato.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Jikombe iliyopo wilayani Chato wakati alipofika shuleni hapo kukagua miundombinu ya shule.
*****************************
Serikali kupitia mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) imetenga takribani shilingi bilioni 201 kwa ajili ya awamu ya nane ya uboreshaji na ujenzi wa miundombinu ya shule nchini
Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako Wilayani Chato wakati wa ziara ya kikazi kukagua utekelezaji wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule za msingi na sekodari zinazokarabatiwa kupitia mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) ambapo amesema suala la ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya shule ni endelevu.
“Ujenzi au uboreshaji wa miundombinu ni suala endelevu na ukiangalia katika kipindi cha uongozi wa Mhe. Rais John Pombe Magufuli katika upande wa miundombinu mpaka sasa kwenye mradi wa EP4R tumeshatumia bilioni 306 ambapo zimefanya ujenzi wa madarasa katika awamu saba, ” amesema Profesa Ndalichako.
Waziri Ndalichako amesema katika awamu ya nane ya Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) kipaumbele kitakuwa kwa Halmashauri ambazo zimepewa fedha na kufanya vizuri katika usimamizi wa fedha katika awamu zilizopita na zile ambazo hazikufanya vizuri zitapatiwa fedha baada ya kushughulikiwa wale wote ambao wamekuwa wakikwamisha utekelezaji wa miradi hiyo.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Chato Charles Kabeho ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutoa fedha zaidi ya Bilioni 1.3 kupitia Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mipya ya shule na ukamilishaji wa maboma yaliyokuwa katika hatua mbalimbali wilayani humo.
“Kwa Kweli fedha hizi zimetusaidia tumeweza kutatua changamoto ya miundombinu iliyojitokeza baada ya sera ya elimu bila malipo kijitokeza,”alisema Mkuu wa Wilaya hiyo
Mhandisi Kabeho amesema wilaya ya Chato itaendelea kuwahamasisha wananchi kuendelea kujitokeza katika kuchangia nguvu kazi katika uboreshaji wa miundombinu ya shule ili kuhakikisha nao wanachingia katika uwekezaji wa elimu bila malipo ili kuwezesha wanafunzi kusoma katika mazingira bora.
Naye Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Jikomboe Valentina Geofrey amemshukuru Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kutimiza ahadi yake aliyoitoa Januari alipotembelea shule hiyo ya kuwajengea ukuta kuzunguka shule pamoja na bwalo la chakula ambavyo kwa kiasi kikubwa vinakwenda kupunguza changamoto ambayo wamekuwa wakikutana nazo. Aidha, Mwanafunzi huyo amemuomba Waziri kuwasaidia kuwajengea maabara za sayansi ili waweze kusoma masomo ya sayansi yatakayowawezesha kushiriki katika azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwa na uchumi wa kati kupitia viwanda.
Naye mmoja wa wazazi Elizabeth Lukanyima ameupongeza uongozi wa serikali ya Awamu ya Tano kwa uboreshaji wa miundombinu ya shule na kuwataka wazazi kuhakikisha wanawasimamia watoto wao ili waweze kupata elimu iliyobora na kuweza kushiriki katika ujenzi wa nchi.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Ndalichako katika ziara yake ya kukagua miradi ya elimu katika Halmashauri ya wilaya ya Chato ametembelea na kukagua ujenzi wa ofisi ya Uthibiti ubora wa shule, ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika shule ya sekondari ya Jikomboe, Bwina na shule ya msingi Chato aliyosoma Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Pamoja na ujenzi wa majengo mapya katika shule ya msingi ya Chato unaofanywa na Mradi wa Lipa kulingana na Matokeo (EP4R), Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa matatu na ofisi mbili za walimu.