Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
MNUFAIKA wa mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF )mtaa wa Miwaleni,kata ya Visiga ,Kibaha Mjini Mkoani Pwani ,Miriam Pazi maarufu mapesa amesema kwa hakika mpango huo umemnufaisha kutoka alipokuwa akilala kwenye kibanda Cha maturubai hadi sasa amejenga nyumba yenye umeme .
Ameeleza mbali ya mafanikio hayo pia yeye na wenzake wameweza kuanzisha kikundi ambacho wameshakusanya milioni 1.4 ambapo wanakopeshana ili kuendeleza miradi yao.
Akielezea namna TASAF ilivyokomboa maisha yake, wakati Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete alipofika , Mtaa wa Miwaleni wakati wa muendelezo wa ziara yake Mkoani Pwani,Miriam alisema kabla ya mpango huo alikuwa na Hali mbaya kimaisha na kiuchumi.
Nae mnufaika mwingine Esther Bilinge alieleza anashukuru TASAF kwa kusomesha watoto wake, kupata uhakika wa chakula na Sasa amenunua shamba na kujenga nyumba ndogo .
Akielezea mradi huo unavyotekelezwa Halmashauri ya Mji Kibaha Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Mshamu Munde alieleza,tangu kuanza kwa mpango Halmashauri imehawilisha Bilioni 1.3 kwa kaya 2,583.
“Kwa Kuwa mpango umeelekeza walengwa kujiunga na malipo kwa njia ya mtandao,Jumla ya kaya 2,168 kati ya kaya 2,480 za walengwa zimeshajiunga na malipo kwa njia za mitandao na kaya 312 bado hazijajiunga na malipo kwa njia hiyo.”alifafanua Munde.
Anaeleza katika malipo ya dirisha la mwezi January/February 2023 Jumla ya milioni 12.777 zililipwa kwa kaya 312 za walengwa wanaolipwa kwa njia ya taslimu na 91,359,608 zililipwa kwa njia ya mitandao ya simu na benki kwa kaya 2,168.
Akizungumza na wakazi wa Miwaleni Ridhiwani alieleza, Bilioni 51 zimepelekwa TASAF kuwezesha na kubadili maisha ya kaya zenye uhitaji.
“Rais dkt.Samia Suluhu Hassan ameonyesha Utayari wa kuendelea kusaidia Watanzania wenye uhitaji ,hivyo takwimu sahihi za walengwa zipatikane,wafikiwe ili mpango ulete matokeo chanya “alifafanua Ridhiwani.
“Watendaji waende nyumba kwa nyumba kubaini wenye uhitaji , tusisubiri kuleta visingizio,janjajanja ili kutosaidia Watanzania hawa,la msingi watambuliwe walengwa bila kuwasubiri wawafuate kwenye mikutano “
Ridhiwani alielezea Watanzania milioni 1.3 wananufaika na TASAF, ni Lazima tuishukuru Serikali kwa jitihada kubwa inayofanya kuhakikisha mpango unatekelezwa na walengwa wanafikiwa.
Aliahidi kuendelea kufanyia kazi kwa kuzitatua changamoto ambazo bado zinaonekana kubainika ili kurahisisha utekelezaji wa Mpango huo uweze kuleta tija kwa jamii.
Pamoja na hayo, Ridhiwani alitoa rai kwa walengwa kwenye mtaa huo kushiriki mikutano ya uhakiki,kwani moja ya changamoto zinazotajwa ni pamoja na walengwa hao kutofika kwenye mikutano ili kufanyiwa uhakiki suala ambalo linasababisha usumbufu kwa watendaji.