Afisa wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Huduma za Kurugenzi ya Ujumuishi na Ustawi wa Huduma za Fedha, Bw. Lucas Maganzi akizungumzia kuhusu mifuko ya mikopo inayosimamiwa na Benki Kuu ya tanzania BoT.
Afisa wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Huduma za Kurugenzi ya Ujumuishi na Ustawi wa Huduma za Fedha, Bw. Lucas Maganzi akizungumza na wageni mbalimbali waliotembelea katika banda la BoT.
Elimu ikiendelea kutolewa na maafisa wa Benki Kuu ya Tanzania wakati walipotembelea katika bana hilo.
NA JOHN BUKUKU, DAR ES SALAAM.
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaendelea kuratibu mifuko miwili kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wakopaji wenye changamoto ya ukosefu wa dhamana.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam katika Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa kwenye viwanja vya Sabasaba barabara ya Kilwa jijini Dar es Saalaam, Afisa wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Huduma za Kurugenzi ya Ujumuishi na Ustawi wa Huduma za Fedha, Bw. Lucas Maganzi, amesema kuwa ni mifuko ya serikali ambayo ipo chini ya BoT.
Amesema kuwa mifuko hiyo inalenga wafanyabiashara wadogo na wakati pamoja na wanafanyabiashara wanaongeza thamani bidhaa zao kwa ajili kwenda kuuza nje ya nchi.
“Ili upate mkopo katika mifuko hiyo unakwenda katika Benki ya Biashara yoyote kwa ajili ya kukufanyiwa tathmini na benki husika, baada ya hapo benki inatoa taarifa BoT kama unakidhi vigezo”
Amesema kuwa kigezo cha kupata mkopo lazima uwe na dhamana yenye thamani asilimia 50 ya kiasi cha fedha ambacho umekusudia kukopa, huku benki ikipewa jukumu la kukufatilia kwa ajili ya marejesho.
Hata hivyo amesema kuwa ili kuhakikisha huduma za fedha zinatambulika kisheria na kufikiwa na watu wanaendelea kuratibu wadau mbalimbali katika sekta ya fedha.
Amesema wadau hao ni Balaza la Taifa la Jumuishi la fedha ambalo Mwenyekiti ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania ambapo huwa wanakutana kwa ajili ya kujadili na kutatua changamoto zilizopo katika sekta ya fedha.
BoT pia wanaratibu na kutoa elimu ya fedha kwa sababu uelewe ni moja ya chachu ya kufanya watu watumie huduma rasmi za fedha baada ya kuwa na uwelewa mkubwa kupitia elimu inayotolewa.