Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imefanya Mkutano wa Dharura kwa njia ya mtandao kwa lengo la kujadili hali ya ulinzi na usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Msumbiji.
Mkutano huo umeongozwa na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe. Netumbo Nandi Ndaitwah ambapo pamoja na mambo mengine, amezisihi Nchi wanachama wa SADC kuendelea kushirikiana na DRC pamoja na Msumbiji na kuhakikisha kuwa hali ya amani inarejea.
“SADC imefanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha inarejesha hali ya amani katika Mashariki ya DRC na Jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji. Hivyo niendelee kuwasihi kuendelea kushirikiana na kuhakikisha hali ya usalama katika nchi hizo inapatikana. Amani na usalama ni bidhaa ghali hivyo yatupasa tuzilinde vyema,” alisema.
Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano katika Mkutano huo uliongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) ambaye ameeleza kuwa Tanzania inatambua na kuthamini mahitaji ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika harakati za kutafuta suluhu ya amani ya kudumu Mashariki mwa DRC na kulaani mashambulizi yanayotekelezwa na makundi ya waasi nchini humo.
“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazidi kulaani vitendo viovu vinavyotekelezwa na vikundi vyenye silaha dhidi ya raia wa DRC wasio na hatia. Hivyo, ni matarajio yetu kuwa mapendekezo yanayowasilishwa kuhusu uanzishwaji wa misheni hii yatasaidia kutatua changamoto hizo za kiusalama katika nchi za DRC na Msumbiji”
Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utafuatiwa na Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (Organ-Troika) na kufuatiwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali utakaofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 11 Julai 2023