Na Mwandishi wetu, Mirerani.
WAZIRI wa Madini Dkt Dotto Mashaka Biteko, ameipongeza kampuni ya wawekezaji wazawa Franone Mining and Gems Company LTD, inayochimba madini ya Tanzanite eneo la kitalu C Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kwa namna inavyofanya kazi kwenye eneo hilo.
Waziri Dkt Biteko ameyasema hayo kwenye ziara yake mji mdogo wa Mirerani, kwa kuzungumza na wadau wa madini ya Tanzanite, kutembelea kitalu C na kukagua ujenzi wa jingo la soko la madini la Tanzanite City.
Amesema kampuni ya Franone Mining and Gems Ltd, baada ya kushinda tenda na kukabidhiwa eneo la kitalu C, imefanya kazi kubwa kwa muda mfupi, kinyume cha matarajio ya watu wengi.
“Tumepata mwekezaji bora kwani aliahidi kuwa ataanza uzalishaji miezi 18 baada ya kupewa leseni ila ndani ya miezi sita ameweza kufanikisha uzalishaji tofauti na malengo ya awali,” amesema Waziri Dkt Biteko.
Amesema kampuni ya Franone imeanza uzalishaji wa madini ya Tanzanite kwenye kipindi ambacho Serikali inahesabu kuwa wapo kwenye usafi na kutengeneza miundombinu ya uchimbaji.
“Kampuni ya Franone Mining ilipewa eneo mgodi ukiwa umechakaa, wakati akifanya ukarabati wa miundombinu yake ya kazi wameshaanza uzalishaji, wanastahili pongezi,” amesema Dkt Biteko.
Kampuni imeajairi watu 328 kwa muda mfupi bado yupo kwenye ujenzi wa miundombinu na Serikali inakusanya kodi kwenye madini, inapata kodi kwenye ajira hivyo muungeni mkono.
“Ni kawaida yetu tunapomuona mwekezaji ni mweusi kama sisi tunadharau badala ya kumuunga mkono, mpeni ushirikiano mtanzania mwenzetu na pia kuna mama wa kimasai alisema mngeleta mgeni nisingeweza kuzungumza naye kiingereza ila Onesmo Mbise hata kimasai anasikia kidoto,” amesema Biteko.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Dkt Suleiman Serera ameipongeza kampuni ya Franone kwa namna inavyosaidia ajira kwenye maeneo yanayozunguka madini ya Tanzanite.
“Pamoja na hayo, wanawake mnayopatiwa udongo wekeni utaratibu wenu vizuri ili msiwe mnagombania huo mchanga na pia vijana mnaowasumbua kina mama wanapokuwa na udongo acheni mara moja,” amesema Dkt Serera.
Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka ameipongeza kampuni ya Franone kwa kushinda zabuni ya kuchimba madini ya Tanzanite, eneo la kitalu C.
“Ni kampuni iliyoshinda kwa sifa stahiki na wanastahili kupewa ushirikiano katika kutimiza malengo yao ya uwekezaji wa machimbo ya madini ya Tanzanite,” amesema Ole Sendeka.
Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Franone Mining Onesmo Mbise amesema awali kulikuwa na changamoto ya wanawake wachekechaji na vijana kuangaika vichakani kufuata udongo ila wakapanga utaratibu wa kuwapa udongo.
Mbise amesema hivi sasa ni mwezi wa nne au watano wanaendelea kuwapa udongo, kupitia malori manne yanayowasogezea udongo wa kuchekecha pindi ukitolewa mgodini.
Mmoja kati ya wanawake wanaosuka kamba za manila kwenye kampuni hiyo, Nai Leyani amemshukuru mkurugenzi wa kampuni hiyo Onesmo Mbise kwa kuwapa ajira.
“Kwa kweli tunamshukuru Mungu kwa kupata ajira kwani hivi sasa, tunasaidiana na wanaume zetu, katika kuhudumia na kutunza familia zetu majumbani kutokana na ajira ya Franone,” amesema Nai.
Mwenyekiti wa wanawake wachekechaji Nadoiwoki Julius, amesema kampuni ya Franone Mining imewasaidia makundi manne ya wanawake, walemavu, wazee na vijana wanaochekecha udongo.
“Tuna imani kubwa na wewe Onesmo Mbise, ila tunaomba tuongezewe udongo, kwani tupo wengi na udongo ni mchache na pia nafasi za ajira zikitokea wanawake tusisahaulike.,” amesema Nadoiwoki.