Na Victor Masangu,Kibaha
Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka ametimiza ahadi yake kwa vitendo baada ya kukamilisha zoezi la kutoa mifuko ya saruji 100 kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa ofisi ya Bakwata iliyopo kata ya kongowe Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani.
Koka ametekeleza kwa vitendo katika halfa fupi ambayo ilifanyika katika eneo la viwanja ambavyo ujenzi huo unafanyika na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa dini ya kiislamamu pamoja na chama cha mapinduzi (CCM) na wananchi kutoka maeneo mbali mbali ya Wilaya ya Kibaha.
Katika halfa hiyo Mbunge huyo alibainisha kwamba ametekeleza ahadi hiyo kwa vitendo ikiwa ni moja ya sadaka yake kwa mwenyezi Mungu na kwamba ataendelea kushirikiana bega kwa bega na wananchi wa dini zote wa Jimbo la Kibaha bila ubaguzi wowote katika kuwatumikia katika nyanja zote.
“Leo nimekuja hapa kongowe mtakumbuka kwamba nilitoa ahadi yangu wakati wa Baraza la iddy na mm hii ni sadaka yangu kwa bakwata pamoja na Mungu pia na nitaendelea kutoa kadiri ya uwezo wangu kwani kila nikitoa na Mungu anazidi kunipa baraka,”alisema Mbunge Koka.
Alisema kuwa katika kuhakikisha kwamba ofisi ya bakwata Wilaya ya Kibaha inakamilika atahakikisha kwamba mbali na kutoa msaada huo wa saruji lakini pia ataendelea kuweka mipango madhubuti ambayo itasaidia katika kukamilisha ujenzi huo.
Koka alisema kuwa kukamilika kwa ujenzi huo utakuwa na faida kubwa wa waumini wa kiislamu katika kuhakikisha wanatimiza wajibu wao ipasavyo na kuwahimiza kushikamana kwa pamoja katika kufanikisha ujenzi huo.
Kadhalika Koka aliwakumbusha waumini wa dini ya kiislamu kuwa na upendo amani ikiwa pamoja na kuendelea kutoa sadaka kwa hali na mali ili kurudisha matendo mazuri kwa Mungu pamoja na kuwaletea maendeleo wananchi.
Kwa Upande wake Sheikh wa Wilaya ya Kibaha Said Mtonda ameshukuru kwa dhati Mbunge huyo kwa utekelezaji wake wa ahadi kwa vitendo kwa kutoa mifuko hiyo ya sarufi ambayo itakuwa ni mkombozi mkubwa katika kufanikisha ujenzi wa ofisi hiyo ya Bakwata.
Aidha alisema Mbunge huyo amekuwa mstari wa mbele katika siku zote za kuhakikisha anashirikiana bega kwa bega katika dini zote ili kuweza kuleta matokeo chanya ya kimaendeleo bila ya kujali itikadi za kidini.
“kiukweli tumekuwa kwa kipindi kirefu tukishirikiana bega kwa bega na Mbunge wetu wa Jimbo la Kibaha mjini katika mabaraza ya Iddy na amekuwa mstari wa mbele katika kutushika mkono na hii leo ametimiza ahadi yake katika kutoa mifuko 100 ya saruji nampongeza sana na Mungu ambariki sana,alisema.
Hivi karibuni Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini wakati wa Baraza la Iddy ambalo lilifanyika katika kata ya kongowe aliahidi kuchangia mifuko ya saruji 100 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Bakwata Wilaya ya Kibaha na ameitekeleza kwa vitendo.