Na Mwandishi wetu, Babati
MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) kwa kushirikiana na vyombo vingine wameahidi kusaidia kutatua kero ya wanyama wakali kutishia maisha na kula mazao na Mifugo ya wananchi katika eneo la hifadhi ya Jamii ya wanyamapori ya Burunge (JUHIBU)
Wakazi wanaoishi katika eneo wameomba TAWA kuwasaidia kuwaondoa fisi, simba na tembo katika makazi yao kwani wanatishia maisha na wamekuwa wakila mazao yao na mifugo huku wakiahidi kuwa wahifadhi na kuacha ujangili.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika katika Kijiji Cha Vilimavitatu kwa kuwashirikisha viongozi wa vijiji, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi wa TAWA Kanda ya Kaskazini ,Privatus Kasisi amesema Mamlaka hiyo, kwa kushirikiana na mamlaka nyingine wakiwepo wawekezaji wa utalii katika eneo hilo, Chemchem association watajitahidi kutatua kero hizo.
Kamishna Msaidizi Kasisi amesema TAWA itajitahidi kuongeza magari ya doria na kufanya haraka kufika katika matukio yenye tishio la usalama katika eneo hilo lakini pia alitaka wananchi kuacha kufanya shughuli za kibinaadamu ikiwepo kulima na kuingiza mifugo maeneo yaliyohifadhiwa kwani inawafanya wanyama kutoka hifadhini na kuvamia maeneo hayo.
“Kama ukilima mahindi ,dengu na Maharage jirani na hifadhi ni wazi wanyama watatoka hifadhini na Kuna kula mazao hayo kwani ni chakula kipya kwao na wakizoea ni vigumu kuwadhibiti mara kwa mara,” amesema.
Amesema hata hivyo maombi ya wananchi kuomba helkopta kufukuza wanyama hao sio ni vigumu kwani vijiji vyao vipo jirani sana na hifadhi na hivyo matumizi helkopta inaweza kuwa changamoto.
“Kule Kusini tulitumia helkopta kwa sababu tembo kwenye makundi makubwa walikuwa vijijini na ni mbali na hifadhi lakini hapa tutaweza kuleta changamoto nyingine,” amesema.
Hata hivyo, amesema viongozi wa JUHIBU WMA, kwenda vijijini kupata takwimu za mahitaji ya vifaa vya kupambana na uvamizi wa anyamapori, kwani taasisi yaChemChem ipo tayari kutoa vifaa ikiwepo tochi, vuvuzela kufukuza wanyama na simu za mkononi ili viongozi waweze kutoa taarifa haraka wanapoona makundi ya wanyama wakali katika maeneo yao.
Kamanda wa Polisi Mkoa Manyara, George Katabazi, amesema jeshi hilo litaendelea kushirikiana na TAWA na vyombo vingi kuhakikisha usalama wa wananchi na kuwataka wananchi nao kuacha kujihusisha na vitendo vya ujangili.
Kamanda Katabazi amesema polisi watajitahidi sana kuzuia wanyamapori kusababisha vifo lakini wananchi pia waache vitendo vya ujangili.
Amesema pia Jeshi hilo kwa kushirikiana na TAWA watajitahidi kuitisha kikao kikubwa ambacho kitashirikisha viongozi wa TANAPA na Wizara ya Maliasili na Utalii ambao wanahusika na malipo ya fidia ili kumaliza migogoro katika eneo hilo.
Mwenyekiti wa kijiji cha Sarawe, Joseph Bura na Mwenyekiti wa kijiji cha Sangaiwe Marian Mwanso na mwananchi Akoonay Mitsay wamesema wanyama wakali wamekuwa kero kubwa kwao na jitihada za vijiji kuwaondoa zimekwama kutokana na ongezeko lao kubwa kwenye makazi ya watu.
“Siku hizi watoto tunalazimika kuwasindikiza asubuhi kuwapeleka shule kwa kuhofia wanyamapori fisi na simba sasa kero hii itaendelea hadi lini?” amehoji Bura.
Kwa upande wake, Mwanso amesema Tembo wamekuwa kero kwani wanakula mazao ya wananchi na sasa wanashindwa kulima.
Mitsay amesema wao wataendelea kuwa wahifadhi wazuri na kuacha ujangili lakini pia serikali iondowe kero ya wanyama wakali katika maeneo yao.
Mwenyekiti wa Kijiji Cha Vilimavitatu, Abubakari Msuya amepongeza TAWA, Jeshi la polisi na mwekezaji Chemchem kwa kufanikisha kikao hicho muhimu.
Msuya amesema yeye binafsi shamba lake hekari 20 zimevamiwa na kuliwa na wanyama na hadi sasa hajui hatima yake.
“Kikao hiki kimekuwa na manufaa na tutapenda Vikao zaidi na kama mlivyoahidi waje pia watu wa Wizarani na TANAPA ili kumaliza migogoro na tunaomba elimu ya uhifadhi iendelee kutolewa vijijini,” amesema.
Mwisho.