Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiweka Jiwe la Msingi ufunguzi wa Hoteli ya Kisasa ya Bwami Dubai iliopo Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma. Kushoto ni Mkurugenzi wa Hoteli hiyo Evance Chocha Bachunya. Tarehe 05 Julai 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Hoteli ya Kisasa ya Bwami Dubai iliopo Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma. (Kutoka kulia ni Naibu Waziri TAMISEMI Deogratius Ndejembi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako, Mke wa Makamu wa Rais Mama Mbonimpaye Mpango Mkurugenzi wa Hoteli hiyo Evance Chocha Bachunya na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye). Tarehe 05 Julai 2023.
…….
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa watanzania hususani wazawa wa Mkoa wa Kigoma kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika mkoa huo ili kuchochea ukuaji wa uchumi.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Hoteli ya Kisasa ya Bwami Dubai iliogharimu shilingi bilioni 1.6 iliojengwa na mzawa wa Kigoma Evance Chocha katika Wilaya ya Kasulu mkoani humo.
Amesema serikali inatambua mchango wa wazawa na wageni kutoka sehemu mbalimbali za nchi na hata nje ya nchi katika kuchochea maendeleo ya mkoa wa Kigoma na Taifa kwa ujumla.
Aidha amewahimiza viongozi wa Serikali ya Mkoa wa Kigoma kuhakikisha wanaweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika mkoa huo ikiwemo kufanya upimaji wa ardhi kwaajili ya biashara na uwekezaji.
Amewasihi wananchi kuangalia vema gharama za ardhi ili kutowapoteza wawekezaji wenye nia ya dhati ya kuwekeza katika mkoa huo.Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hoteli ya Bwami Dubai , Evance Chocha amesema uwekezaji wa hoteli hiyo umechagizwa na sera za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Chama cha Mapinduzi.
Amesema uwepo wa hoteli hiyo umeweza kuongeza ajira katika eneo la Kasulu na kuinua maisha ya wananchi wa eneo hilo.
Hoteli hiyo imeahidi kuchangia mifuko ya saruji 500 katika shule ya watoto wenye mahitaji maalum ya kalema.Katika hatua nyingine akipokea changamoto mbalimbali za wananchi wa Wilaya ya Kasulu, Makamu wa Rais ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuharakisha uwekaji mipaka katika hifadhi ya Kagerankanda ili kuepusha migogoro inayojitokeza baina ya wananchi na hifadhi.
Aidha amewataka wananchi wa eneo hilo kuheshimu na kutambua umuhimu wa uhifadhi wa rasilimali unaofanywa na serikali kwani ni lengo la kuhakikisha zinakuwa endelevu kwa taifa.
Amesema rasilimali hizo ikiwemo hifadhi ya Kagerankanda ndio chanzo cha utalii na upatikanaji wa mvua hivyo serikali inaendelea na utaratibu wa kupanga matumizi ya ardhi kwa maslahi ya taifa ya sasa na baadae.
Pia Makamu wa Rais amemuagiza Waziri wa Maji kuhakikisha anamaliza changamoto ya maji katika eneo la Kasulu hususani vijiji vya Juhudi, Nyantale na Mdyanda ambavyo tayari visima vimechimbwa tangu mwaka 2021.
Pia ameagiza kushughulikiwa kwa tatizo la kukatika umeme katika mji huo pamoja na upungufu wa walimu unaoikabili wilaya ya Kasulu.
Halikadhalika Makamu wa Rais amewahimiza wafanyabiashara na Wawekezaji katika eneo la Kasulu na maeneo mbalimbali ya nchi kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari na kuzingatia utoaji wa risiti za kielekroniki.
Pia amewasisitiza wananchi hao kulinda na kuhifadhi mazingira. Amesma shughuli zote za kiuchumi na kijamii ni lazima zizingatie utunzaji na uhifadhi wa mazingira.
Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa Kigoma kuacha tabia za kuchoma moto ovyo hususani kipindi cha kiangazi na kuwaagiza Viongozi kuchukua hatua kali za kisheria kwa yeyote atakayehusika.
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais 05 Julai 2023Kasulu, Kigoma.