Na Mwandishi wetu
Mapambano dhidi ya udanganyifu kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ni jukumu la msingi lililoshika kasi hasa kutokana na kuongezeka kwa viashiria vya udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wadau wasio waaminifu. Hili limepelekea Mfuko kubuni mbinu mbalimbali za kubana mianya na kuchukua hatua stahiki kwa wanaobainika.
Hayo yameripotiwa na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Bw. Bernard Konga alipokuwa akiwasilisha mada katika Mkutano wa Wadau wake uliofanyika Mtwara leo.
Akiwasilisha mada hiyo amesema Mfuko umejipanga na unaendelea kubuni mbinu za kukabiliana na udanganyifu unaofanywa na wachache wenye nia ya kuuhujumu kwa manufaa yao yasiyo halali.
“Tunabaini udanganyifu na tunachukua hatua ili Mfuko huu uendelee na kiwanufaisha watanzania lakini pia tunachukua hatua kwa wanaobaika” amesema Bw. Konga.
Amesema kuwa Mfuko umeshafungia vituo takriban 20 katika mwaka 2022/23 kutokana na kubainika na udanganyifu kwa Mfuko na unaendelea kuchukua hatua ikiwa ni kuvifikisha katika mamlaka husika.
Amesema hatua nyingine ni kuimarisha uhakiki wa wanachama kwenye vituo vya huduma ili kuhakikisha wanachama sahihi wanatibiwa.
“Tumeanza majaribio ya kutumia alama za kibaolojia za vidole na uso katika kuhakiki wanachama na tunatarajia kuanza utaratibu huu kwa vituo vyote kuanzia mwezi Agosti” amesema Bw. Konga.
Ametumia mkutano huu kuutahadharisha umma hususan wadau wake kujiepusha na vitendo vya udanganyifu kwa kuwa sasa Mfuko unachukua hatua kali dhidi ya mtu yeyote atakayejihusisha na vitendo vya udanganyifu.
Amesisitiza kuwa madhara ya kujihusisha na vitendo vya udanganyifu sasa yanaweza kuathiri maisha ya mtu kwa kuwa hatua zinazochukuliwa ni za kisheria zaidi ambazo ni pamoja na kufungiwa huduma na kufikishwa katika mamlaka za kisheria.
“Tunafanya kazi na vituo kwa karibu sana, lakini kuna baadhi ya watumishi wenyewe wa vituo vya matibabu wanajihusisha na vitendo vya udanganyifu. Tutafika ili kufanya kaguzi kujiridhisha mazingira yaliyopo kwa watoa huduma tunaofanya nao kazi” Alisema Konga.
Ametoa rai kwa watoa huduma kuona kuwa Mfuko huu ni wa watanzania na ni jukumu letu sote kuulinda na kusisitiza vituo kusaidia kukamata watu wote wanaojihusisha na wizi dhidi ya Mfuko.
Awali akifungua mkutano huo, mgeni rasmi Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF Bw. Juma Muhimbi aliwataka wadau kuwa huru katika kutoa maoni na ushauri kwa Mfuko huu kwa kuwa ni wa manufaa kwa wadau wote.
“NHIF ni ya kwetu wote hivyo tuwe huru kuchangia maoni na kushauri ili kuleta uimara na uendelevu wa Mfuko” amesema Bw. Muhimbi
NHIF imeendelea na mikutano ya wadau kila mwaka ambayo imekuwa ikitoa nafasi kwa wadau kuchangia maendeleo ya Mfuko huo.