………
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza kuwa ifikapo Oktoba mwaka huu, mradi wa majengo ya wizara mbalimbali unaoendelea katika mji wa Serikali uwe umekamilika na kuwekwa samani, ili azma ya Serikali ya watumishi kuhamia kwenye majengo hayo ifikapo Januari Mosi, 2024 itimie
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa mradi huo wahakikishe wananunua bidhaa zinazozalishwa na viwanda vilivyopo nchini lengo likiwa ni kuokoa fedha za kigeni pamoja na kuongeza tija katika uwekezaji.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumatatu, Julai 03, 2023) baada ya kukagua ujenzi wa Mji wa Serikali na uwanja wa Mashujaa, Mtumba jijini Dodoma. “Dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kutaka kuona watumishi wote waliohamia Dodoma wanafanya kazi kwenye majengo rasmi.”
“Tafuteni mbinu za kiufundi za kukamilisha majengo haya kwa wakati bila kuathiri viwango ikiwa ni pamoja na kusimamia ujenzi huu usiku na mchana, tunataka tumalize majengo haya, Watanzania wanataka kuona majengo yanakamilika na kutumika.”
Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wasimamizi wa ujenzi wa mradi huo watumie bidhaa zinazozalishwa na viwanda vilivyopo nchini. “Rais Dkt. Samia amesisitiza kuhusu uwekezaji na amekuwa akialika wawekezaji wa nje na wa ndani kujenga viwanda vya bidhaa mbalimbali hapa nchini ikiwemo marumaru (tiles). Tutumie bidhaa zao badala ya kuagiza bidhaa hizo kutoka nje.”
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama amesema mbali na mradi wa ujenzi wa majengo ya wizara pia mradi mwingine unaotekelezwa katika eneo hilo ni ujenzi wa uwanja wa Mashujaa ambao utakuwa na mnara utakaoongoza kwa urefu barani Afrika. Mnara huo utakuwa na urefu wa mita 110.
Awali, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi alisema watahakikisha wanasimamia kikamilifu ujenzi wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili. “Ifikapo Septemba 30, 2023 mradi huo utakuwa umekamilika.”