……..
MWENYEKITI aliyemaliza muda wa uongozi katika Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Ndg. Abdulrahman Kinana, ametunukiwa nishani ya uongozi bora wa kipindi cha mwaka mmoja alipokuwa mwenyekiti wa taasisi hiyo.
Nishani hiyo imekabidhiwa kwa niaba ya Viongozi wakuu wa Vyama wanachama Wa TCD na Mwenyekiti mpya wa TCD, Profesa Ibrahim Lipumba, katika mkutano wa viongozi wakuu wa vyama wanachama wa TCD, uliofanyika Julai 3, 2023, katika ofisi za TCD, Dar es Salaam.
Kabla ya kumkabidhi nishani hiyo, Profesa Lipumba ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF, alisema kuimarika kwa TCD kwa sasa kunatokana na mchango wa kipekee wa Ndg. Kinana ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi.
“Kwa niaba ya wakuu wenzangu wa vyama vya siasa wanachama wa TCD, uongozi Ndg. Kinana umetuwezesha kutuunganisha sisi wote, tunakukabidhi nishani hii iwe kumbukumbu kwa kazi yako nzuri, asante sana,” alisema Profesa Lipumba.
Viongozi wengine wa vyama vya siasa ambavyo ni wanachama wa TCD waliohudhuria mkutano huo na kushuhudia Ndg. Kinana akitunukiwa nishani hiyo ni Mwenyekiti wa Chadema, Ndg. Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Haji Ambar, Mwenyekiti wa CHAUMMA, Ndg. Hashim Rungwe, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Juma Duni Haji pamoja na Makatibu Wa Kuu wa Vyama hivyo.
Ndg. Kinana alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa TCD, Aprili mwaka 2022 kwa kipindi cha miezi sita, na baadaye wakuu hao wa vyama walimuongezea muda wa uongozi kwa kipindi kingine cha miezi sita baada ya kufanyika marekebisho ya katiba ya TCD.
Kikao kilimchagua Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Ndg. Ambar kuwa Makamu Mwenyekiti wa TCD.