Na. Damian Kunambi, Njombe
Waziri wa Utamaduni, sanaa na michezo Balozi Dkt. Pindi Chana, ameziagiza halmashauri zote hapa nchini kuhakikisha zinatenga maeneo kwaajili ya viwanja vya michezo mashuleni ili wanafunzi waweza kukuza vipaji sambamba na kujenga afya zao.
Waziri Chana ameyasema hayo mara baada ya kuwasili katika shule ya sekondari Madilu iliyopo Wilayani Ludewa mkoani Njombe kwa lengo la kukabidhi msaada wa bati 152 zenye thamani ya zaidi ya sh. Mil 5.
Amesema wanafunzi wawapo mashuleni wanapaswa kushiriki michezo mbalimbali ambapo katika kusapoti hilo aliwakabidhi mipira miwili wanafunzi wa shule ya Madilu ambapo mmoja kwaajili ya wanafunzi wa kiume na mwingine kwa wanafunzi wa kike.
Sanjali na hilo pia ameviasa vikundi mbalimbali vya sanaa hapa nchini kujisajili katika Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) ili viweze kupata fursa mbalimbali ikiwemo mikopo.
“Mkijisajili mtaweza kutambulika na mtafungua milango ya fursa mbalimbali kama kupatiwa mikopo, kupata mialiko ndani na nje ya nchi pamoja na fursa nyingine nyingi ambazo hamkuwahi kuzipata hivyo fikeni kwa maafisa utamaduni waliopo katika halmashauri zenu muweze kupatiwa utaratibu” Amesems Dkt. Pindi Chana.