Na WAF- Morogoro.
NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewapongeza wachezaji wa kandanda Dickson Job pamoja na Kibwana Shomari wa Timu ya Yanga kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha huduma za afya kwa wananchi hasa katika eneo la afya ya mama na mtoto kwa kutoa vitanda vya kulaza wagonjwa 10 pamoja na vyandarua vyenye dawa zaidi ya 100 kupitia kampeni yao ya Wape Tabasamu.
Dkt. Mollel amesema hayo wakati akikabidhi vifaa hivyo kwa Mwenyekiti wa Halmashauri ambaye aliwakabidhi Mganga Mkuu wa Wilaya pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri, tukio lililofanyika katika kituo cha afya Mkuyuni Mkoani Morogoro, na kuhudhuriwa na Mbunge wao Mhe. Hamisi Tale Tale.
Serikali ya Rais wetu Mge. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye mkoa wa Morogoro imeleta zaidi ya Bilioni 31 kwaajili ya kuboresha huduma ikiwemo ujenzi wa miundombinu, ambapo zimejenga hospitali 6 za wilaya, zahanati 96 ma vituo vya afya 22, huku akitoa zaidi ya Bilioni 11 kwenye eneo la vifaa tiba na dawa, hivyo kufanya kuwa Bilioni 42 katika eneo ka afya tu.
“Pamoja na kazi kubwa mnayotufanyia ya kutuchangishia fedha kwaajili ya kuboresha huduma ya afya ya mama na mtoto, lakini Rais wenu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye mkoa wa Morogoro emeleta zaidi ya Bilioni 31 kwaajili ya kuboresha huduma ikiwemo ujenzi wa miundombinu, ambapo zimejenga hospitali 6 za wilaya, zahanati 96 ma vituo vya afya 22,” Amesema.
Sambamba na hayo, amewapongeza watoa huduma kwa juhudi wanazofanya za kuwahudumia wananchi katika eneo la Makuyuni, na kusisitiza Rais Samia anatambua mchango mkubwa wanaofanya na ataendelea kutatua changamoto zao ikiwemo upungufu wa Watumishi katika kituo hicho.
Nae, Mbunge wa Morogoro Mhe. Hamis Tale Tale amewapongeza wachezaji Dickson Job pamoja na Kibwana Shomari kwa moyo wa kipekee uliowapelekea kuja katika kituo cha afya Mkuyuni na King’oli kujionea mapungufu katika vituo hivyo nakuleta vitanda pamoja na vyandarua ili kusaidia kuboresha huduma kwa wananchi.
Pia, amewapongeza wananchi kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali, na kusisitiza kuwa, hatowaangusha katika kuwatumikia ili kuleta maendeleo katika jimbo hilo.