Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Hamis Mwinjuma amefungua na kufunga mbio za masafa marefu za kiswahili (Swahili Marathon) zilizofanyika jijini Arusha tarehe 1/7/2023 ikiwa ni kuelekea Kilele cha Siku ya Kiswahili Duniani Julai 7, 2023
Akizungumza baada ya kushiriki na kuongoza mbio za km 5, Mhe. Mwinjuma amesema mbio hizo zina lengo la kuleta ari na mwamko kwa Watanzania, Afrika na Duniani kote ili kuyapa hadhi maadhimisho ya siku ya Kiswahili Duniani.
Mhe. Mwinjuma ameongeza kuwa mbio hizo zinalenga kuchochea na kuendeleza juhudi za kutangaza utalii wa Tanzania ambazo zilianzishwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuru ya Muungano wa Tanzania kupitia filamu aliyoianzisha ya Royal Tour.
Mhe. Mwinjuma amesema lugha ya Kiswahili ndio chombo kinachounganisha Watanzania wote na makabila 120 hivyo amewaomba Watanzania kuonesha Uzalendo kupitia lugha ya Kiswahili kwa kushiriki matukio kama hayo ambayo yanazidi kukitangaza Kiswahili Duniani kote.