Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akifanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Uturuki Mheshimiwa Balozi Idd Seif Bakari,mazungumzo yaliofanyika Jijini Dodoma leo tarehe 30 Juni 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Uturuki Mheshimiwa Balozi Idd Seif Bakari mara baada ya mazungumzo yao yaliofanyika Jijini Dodoma leo tarehe 30 Juni 2023.
……..
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo tarehe 30 Juni 2023 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Uturuki Mheshimiwa Balozi Idd Seif Bakari, mazungumzo yaliofanyika Jijini Dodoma.
Makamu wa Rais amempongeza Balozi Bakari kwa kuaminiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwenda kuiwakilisha Tanzania na watu wake katika taifa la Uturuki.
Amemuagiza kuhakikisha anakuwa na nyenzo muhimu zinazobeba vipaumbele vya nchi kama vile Dira ya Maendeleo ya Taifa, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020.
Amemsihi Balozi Bakari kuhakikisha anatekeleza diplomasia ya uchumi ikiwemo kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa Tanzania pamoja na kutafuta wawekezaji hususani katika maeneo ya kipaumbele na kuwatafutia fursa wafanyabiashara na wananchi wa Tanzania kwa ujumla.
Amemsihi balozi huyo kuendeleza na kukuza mahusiano baina ya Tanzania na nchi ya Uturuki kwa manufaa ya pande zote mbili.
Makamu wa Rais amemuagiza Balozi Bakari kuhakikisha anashiriki katika mikutano mbalimbali itakayowezesha kujifunza, kueleza mazuri ya Tanzania pamoja na kutangaza utalii.
Amesema ni vema kuendelea kuitafutia fursa na kuitangaza lugha ya Kiswahili,utamaduni, Sanaa na michezo ya Tanzania.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema ni muhimu kwa Balozi huyo kufanya jitihada za makusudi kuifahamu vema nchi anayokwenda kuiwakilisha Tanzania ili kuweza kujifunza misingi ya ukuzaji wa uchumi wao na kuhamisha maarifa hayo kwa taifa la Tanzania. Pia amemuagiza kuwaunganisha watanzania wanaoishi Uturuki ili waweze kuchangia vema maendeleo ya Tanzania.
Kwa upande wake Balozi Idd Seif Bakari ametaja fursa zinazotokana na Ushirikiano baina ya Tanzania na Uturuki ikiwa ni pamoja na kuuza mazao nchini Uturuki kama vile Pamba, Kahawa, Chai na Tumbaku.
Amesema kutokana na Uturuki kuendelea kwenye sekta ya viwanda vya nguo Ubalozi huo unatarajia kuongeza soko la mazao na kuhakikisha wawekezaji wa Uturuki wanawekeza Tanzania na kuongeza thamani ya mazao hapa hapa nchini.
Ameongeza kwamba Ubalozi unatarajia kuweka mkakati wa kukuza utalii kupitia Shirika la Ndege la Uturuki kwa kutangaza vivutio vya utalii walau wakati wa kuruka na kutua ndege hizo.Imetolewa naOfisi ya Makamu wa Rais30 Juni 2023