Mkurugenzi wa Uendelezaji Biashara wa TBL Group,Bruno akieleza ujumbe wa Balozi wa Japan jinsi kampuni inavyoendesha shughuli zake.
Balozi wa Japan nchini na ujumbe wake wakipata maelezo kutoka Mkurugenzi wa Ufundi wa TBL, Jemedari Waziri.
Meneja Usalama na Afya mahali pa kazi wa TBL,Revocatus Rutakwa akieleza ujumbe wa balozi kuhusu kampuni inavyozingatia usalama wakati wote.
Ujumbe wa Balozi wa japan nchini,ukifuatilia maelezo kutoka kwa wataalamu wa TBL wakati wa ziara hiyo.
……………………..
Balozi wa Japan nchini Tanzania, Shinichi Goto,amefanya ziara katika kiwanda cha bia Tanzania Breweries Limited (TBL), kilichopo Ilala, Dar es Salaam. Aliongozana na ujumbe wa Maofisa wa ubalozi huo, ambapo waliweza kupata taarifa za uwekezaji nchini, utendaji kazi wa kampuni sambamba na kutembelea kiwanda cha kutengeneza bia.
Katika ziara hiyo, Balozi Goto, alipata maelezo ya jinsi kampuni ya TBL Group chini ya kampuni mama ya kimataifa ya ABInBEV, inavyoendesha biashara zake sambamba na kuunga mkono jitihada za serikali katika kufanikisha Malengo Endelevu ya Dunia (SDGS’s).
Mkurugenzi wa Uendelezaji Biashara wa TBL Group, Bruno Zambrano, aliueleza ujumbe huo wa Balozi Guto, jitihada zinazofanywa na kampuni kutekeleza masuala hayo kwa lengo lakuifanya jamii kuwa na maisha bora na endelevu katika maeneo ya kusaidia miradi ya maji salama, kuhamasisha matumizi mazuri ya maji, utunzaji wa mazingira, kuwezesha wanawake kiuchumi, kutoa elimu ya ujasiriamali sambamba na elimu ya unywaji wa kistaarabu, kuwezesha wakulima wadogo wanaoiuzia kampuni malighafi na kutoa ajira nyingi kwa wananchi wa Tanzania kupitia mtandao wa biashara zake.
Zambrano, pia alieleza kuwa TBL imekuwa mstari wa mbele kuchangia pato la serikali kwa njia ya kulipa kodi ambapo imeweza kutunukiwa tuzo ya Mlipa Kodi Bora nchini na tuzo nyinginezo baadhi yake zikiwa tuzo ya Rais ya Mzalishaji Bora na tuzo ya Mwajiri bora.
Balozi wa Japan nchini, Shinichi Goto na ujumbe wake waliipongeza TBL kwa jitihada inazofanya kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta ya viwanda sambamba na uwekezaji katika teknolojia za kisasa na mifumo ya kisasa ya uendeshaji viwanda kwa ufanisi wa kimataifa.
Mkurugenzi wa Ufundi wa TBL, Jemedari Waziri, alisema “TBL inawashukuru kwa ziara yenu hapa kiwandani na kuweza kuona tulikiendelea na jitihada za kuchangia kukuza uchumi wa Tanzania, kupitia uwekezaji wetu katika sekta ya viwanda na kilimo sambamba na kulenga kunufaisha makundi mbalimbali katika jamii. Tutaendelea kuongeza uwekezaji zaidi”.
Waziri, alisema kampuni imejipanga kuhakikisha inafanya uwekezaji mkubwa wa matumizi wa teknolojia za kisasa na kuwa na wataalamu ili kuhakikisha inazalisha bidhaa bora kwa gharama nafuu ikiwa ni moja ya mkakati wa kufanikisha mkakati wa serikali ya awamu ya tano wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.