Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Neema Maghembe akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas alipofanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akitoa maagizo baada ya kutoridhishwa na utekelezaji wa miradi katika Halmashauri ya wilaya ya Songea baada ya kukagua miradi ya vyoo katika shule ya msingi Parangu na mradi wa ukarabati wa Kituo cha Walimu Peramiho iliyogharimu shilingi milioni 57,Mkuu wa Mkoa ameiagiza TAKUKURU kuchunguza miradi hiyo na kuchukua hatua kwa yeyote atakayebainika kuwa na kosa
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Neema Maghembe akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas alipofanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo
Mradi wa ujenzi wa madarasa ya awali katika kijiji cha Mpitimbi wilayani Songea ambapo serikali imetoa shilingi milioni 61 kutekeleza mradi huo wa uboreshajhi elimu ya awali na Msingi (BOOST) ambapo Halmashauri ya Songea imepewa zaidi ya shilingi milioni 700 kutekeleza mradi wa BOOST.
…………………………….
Na Albano Midelo,Songea
SERIKALI imetoa zaidi ya shilingi bilioni sita kutekeleza miradi mbalimbali
ya maendeleo katika Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma
katika mwaka wa fedha wa 2022/2023.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya
Songea Neema Maghembe wakati anatoa taarifa ya utekelezaji wa miradi
hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas alipofanya
ziara ya ukaguzi wa miradi katika Halmashauri hiyo.
Maghembe amebainisha kuwa kati ya fedha hizo,Halmashauri imepokea
zaidi ya shilingi milioni 735 kwa ajili ya mradi wa uboreshaji miundombinu
ya awali na msingi (BOOST),mradi wa vyoo (SWASHI) zimetolewa zaidi ya
shilingi milioni 278 na na mradi wa ujenzi wa madarasa ya awali ya mfano
(LANES) zimetolewa zaidi ya shilingi milioni 55.
“Halmashauri inapenda kuishukuru serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa namna
inavyoendelea kuleta fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo katika
Halmashauri yetu’’,alisema Maghembe.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo,Halmashauri hiyo pia imepokea zaidi ya
shilingi milioni 637 kwa ajili ya umaliziaji wa vyumba vya madarasa katika
shule za msingi,zaidi ya shilingi milioni 75 kwa ajili ya ukamilishaji wa
miradi ya maendeleo vijijini na kwamba serikali pia imetoa shilingi milioni
440 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi.
Kulingana na Mkurugenzi huyo,serikali imetoa shilingi milioni 250 kwa ajili
ya ujenzi wa shule mpya ya msingi Lizabon na shilingi milioni 100 kwa ajili
ya ujenzi na ukarabati wa vyumba vya madarasa na vyoo.
Fedha nyingine zilizotolewa na serikali katika Halmashauri hiyo ni zaidi ya
shilingi milioni 155 ambazo zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya
walimu,zaidi ya shilingi milioni 142 kwa ajili ya ujenzi wa bweni sekondari
ya Darajambili na chuo cha ufundi Liganga.
Maghembe amezitaja fedha nyingine zilizotolewa ni zaidi ya shilingi milioni
278 kwa ajili ya ujenzi wa vyoo shule za msingi,zaidi ya milioni 362 kwa
ajili ya ujenzi wa madarasa,mabweni na vyoo,milioni 834 kwa ajili ya ujenzi
wa vyumba vya madarasa 12,mabweni na vyoo .
Amesema serikali pia imetoa zaidi ya shilingi milioni 751 kwa ajili ya ujenzi
wa vyumba vya madarasa ,mabweni na matundu ya vyoo katika sekondari
ya Mpitimbi na shilingi bilioni moja zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa chuo
cha wenye ulemavu Kata ya Liganga.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas
amekagua mradi wa vyoo katika shule ya msingi Parangu uliogharimu
shilingi milioni 37,mradi wa ukarabati Kituo cha Walimu (TRC) cha
Peramiho kilichogharimu shilingi milioni 22 na mradi wa vyumba vya
madarasa ya awali yaliyogharimu shilingi milioni 61 katika Kijiji cha
Mpitimbi.
Akizungumza baada ya ukaguzi wa miradi hiyo,Mkuu wa Mkoa wa
Ruvuma amepongeza mradi wa ujenzi wa madarasa ya awali katika Kijiji
cha Mpitimbi ambapo ametoa rai kwa wananchi kulinda na kusimamia
mradi huo ili uweze kukamilika kwa asilimia 100.
Hata hivyo Kanali Laban hajaridhishwa na utekelezaji wa miradi ya vyoo
katika shule ya Parangu na ukarabati wa Kituo cha walimu Peramiho
ambapo ameiagiza TAKUKURU kufanya uchunguzi wa kina katika miradi
hiyo na kuchukua hatua kwa mtumishi yeyote atakayebainika kuwa na
kosa.
Amewataka viongozi kuanzia ngazi ya Kijiji,Kata,Tarafa na Wilaya
kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali badala ya kusubiri ziara za
viongozi wa Mkoa kufutilia miradi hali inayosababisha miradi kutekelezwa
chini ya kiwango.
Amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo Neema
Maghembe kuwaandikia barua ya onyo na hatua za kinidhamu zichukuliwe
kwa waandisi wote wanaosimamia miradi kwa sababu wameshindwa
kusimamia miradi.