Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Hassan Masala akimkabidhi cheti maalum Nahonda Josiah Mwakibuja cha kutambua mchango wake katika mazoezi mbalimbali aliyoshiriki wakati Mkuu wa Wilaya huyo alipofunga maadhimisho ya mabaharia yaliyofanyika kitaifa Mkoani Mwanza kuanzia 22-25 Juni 2023.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Hassan Masala akisisitiza jambo kwa wadau na wananchi wa mkoa wa Mwanza (hawapo pichani) wakati alipofunga maadhimisho ya mabaharia yaliyofanyika kitaifa Mkoani Mwanza kuanzia 22-25 Juni 2023.
Mkurugenzi wa Idara ya Usalama na Mazingira wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi-Uchukuzi, Bi. Stela Katondo akisisitiza jambo kwa wadau na wananchi wa mkoa wa Mwanza (hawapo pichani) wakati wa kufunga maadhimisho ya mabaharia yaliyofanyika kitaifa Mkoani Mwanza kuanzia 22-25 Juni 2023.
Baadhi ya Wakuu wa Taasisi mbalimbali za Serikali na wadau wa Sekta ya Bahari wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Hassan Masala akisisitiza (hawapo pichani) wakati alipofunga maadhimisho ya mabaharia yaliyofanyika kitaifa Mkoani Mwanza kuanzia 22-25 Juni 2023.
…………
Serikali imezitaka taasisi zinazoshughulika na masuala ya bahari, Viongozi wa Mikoa inayozunguka Ziwa Viktoria na wadau wengine hususani Mwanza kuhakikisha kunakuwa na mazingira bora kwa ajili ya utunzaji na uteketezaji wa taka ngumu zitakazozalishwa katika Ziwa hilo ili kutoathiri viumbe hai ziwani.
Kauli hiyo imetolewa jijini Mwanza na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Hassan Masala wakati wa akihitimisha maonesho ya siku ya nne (4) ya Mabaharia Duniani yaliyofanyika jijini humo yaliyoshirika Wizara husika kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na taasisi mahususi zinazosimamia masuala ya bahari.
Mhe. Masala amesisitiza kuwa uwekezaji unaofanywa na Serikali na Sekta binafsi hususani kwenye ujenzi wa meli utaongeza uzalishaji wa taka ngumu ambapo bila kujipanga mapema vyombo vya majini vinaweza kuwa na changamoto za kuharibika mara kwa mara na hivyo kuhafifisha uwekezaji huo.
“Mikataba mbalimbali ya kimataifa inayoongoza usafiri wa majini unasisitiza umuhimu wa kutunza mazingira na ikumbukwe kuwa mikataba hiyo ya kimataifa sisi kama nchi tumeridhia na kuiweka kulingana na mazingira yetu hivyo hatuwezi kukwepa kutunza mazingira ili kunusuru viumbe wengine wali nje ya nchi kavu’ Amesema Mkuu wa Wilaya Mhe. Massala.
Mhe. Massala amesema Serikali inaendelea kujenga mazingira mazuri kwa mabaharia wanaohitimu kwa kuzungumza na mashirika mbalimbali ya meli ili kuwawezesha wataalam hao kupata sifa stahiki zitakazowawezsha kufanya kazi ndani na nje ya nchi.Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Usalama na Mazingira, Bi. Stela Katondo amesema Wizara kupitia chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) inaendelea kuboresha mitaala na kuongeza kozi mbalimbali ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje hususani kwenye sekta ya bahari.
Mkurugenzi Katondo ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutenga fedha kila mwaka ili kuboresha miundombinu ya bandari, kujenga na kukarabati meli ili kuifanya sekta hiyo kuchagiza uchumi wa taifa kupitia sekta hiyo ya bahari kwa bahari na Maziwa yaliyopo nchini.
Maadhimisho ya siku ya maharia huadhimishwa mwezi Juni kila mwaka ambapo kwa mwaka 2023 maadhimisho hayo yamebeba kauli mbiu ya “Miaka 50 ya MARPOL uwajibikaji wetu unaendelea” na yamehusisha mazoezi mbalimbali ya uokozi katika ziwa viktoria na utoaji wa elimu ya masuala mbalimbali ya kuzingatia kwa wadau mbalimbali wakiwemo wamiliki wa meli, watumiaji na waendeshaji meli.Imetolewa na kitengo cha habari na mawasiliano Serikalini Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi