Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mbeya ACP Benjamin Kuzaga.
Taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi wa kampuni ya “Giant Tanzania Printers Ltd” iliyopo Jijini Dar es Salaam ndugu DEOGRATIUS ALPHONCE MAGUBO kilichotokea Juni 21, 2023 akiwa amelala katika nyumba ya kulala wageni iitwayo DICCO INN iliyopo maeneo ya Iyunga Jijini Mbeya kwamba sio cha kawaida.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeona taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi wa kampuni ya “Giant Tanzania Printers Ltd” iliyopo Jijini Dar es Salaam ndugu DEOGRATIUS ALPHONCE MAGUBO kilichotokea Juni 21, 2023 akiwa amelala katika nyumba ya kulala wageni iitwayo DICCO INN iliyopo maeneo ya Iyunga Jijini Mbeya kwamba sio cha kawaida.
Ni kwamba Juni 19, 2023 majira ya saa 9:00 usiku, DEOGRATIUS ALPHONCE MAGUBO alifika katika nyumba ya kulala wageni iitwayo DICCO INN akitokea Jijini Dar es Salaam na kuingia kwenye chumba namba 208.
Juni 21, 2023 majira ya saa 5:40 asubuhi, zilipokelewa taarifa katika kituo kikuu cha Polisi Mbeya (Central Police Station) kutoka kwa Meneja wa nyumba hiyo ya kulala wageni kwamba huko katika nyumba ya kulala wageni iitwayo DICCO INN katika chumba namba 208 kuna mteja aliyetambulika kwa jina laDEOGRATIUS ALPHONCE MAGUBO hajaamka mpaka muda huo.
Timu ya makachero wa Jeshi la Polisi ikiongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Wilaya ya Mbeya akiwa ameongozana na kiongozi wa Mtaa huo ilifika eneo la tukio na kuanza kugonga mlango bila mafanikio yoyote hivyo kulazimika kuvunja mlango wa chumba hicho uliokuwa umefungwa kwa ndani na kumkuta DEOGRATIUS ALPHONCE MAGUBO amefariki dunia akiwa amelala kitandani
Uchunguzi uliofanyika katika chumba hicho mbele ya kiongozi wa Mtaa ulikuta dawa mbalimbali za binadamu, Haloxen 1.5, Haloperidol Injection BP, Valparin Chrono 500, Cough Mixer Syrup pamoja na chupa tupu ya pombe aina ya Grants 750ml, Glass ndani yake ikiwa na vipande vitatu vya limao.
Katika uchunguzi huo uliofanywa na Jeshi la Polisi katika chumba alichokuwa amepanga marehemu umebaini kuwa hakuna kitu kingine kinachotiliwa mashaka.
Aidha, Juni 24, 2023 mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi na Daktari Mtaalamu wa Upasuaji (Pathologist) wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya mbele ya ndugu wa marehemu na kuchukua sampuli za mwili wa marehemu na kutumwa kwa wakala wa Mkemia Mkuu wa Serikali Jijini Dar es Salaam kwa uchunguzi zaidi.Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linasubiri matokeo ya uchunguzi na majibu ya Wakala wa Mkemi Mkuu wa Serikali kulinganisha na majibu ya Daktari Mtaalamu wa Upasuaji (Pathologist) ili kuthibitisha kifo cha DEOGRATIUS ALPHONCE MAGUBO ikilinganishwa na uchunguzi wa awali uliopatikana kwenye chumba alichokuwa amepanga.
Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa mtu yeyote mwenye ushahidi mwingine mbali na ushahidi wa kisayansi uliokusanywa asisite kuuwasilisha badala ya kuendekeza taarifa za hisia kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii
Imetolewa na: BENJAMIN KUZAGA – ACP Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mbeya.