KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo ametoa wito kwa wananchi wa Dodoma na wanao zunguka skimu za umwagiliaji kutouza maeneo yao.
Chongolo ametoa wito huo alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa Shina namba 18, Tawi la CCM Bahi Sokoni, wilayani Bahi baada ya Katibu wa shina hilo, Joseph Chipule, alipomueleza kuhusu changamoto ya ubovu wa miundombinu ya skimu za umwagiliaji.
“Wakati Serikali inaweka fedha za kuboresha miundombinu ya skimu za umwagiliaji wajanja wanaotafuta fursa wengi watakimbilia hapa kutafuta maeneo acheni kuuza maeneo ya mashamba yenu, yamilikini endeleeni kuyasimamia mtu akitaka kulima mkodishe alime akupe chako mwaka unaofuata ulime mwenyewe.”
“Kuuza ardhi ambayo imeshawekewa miundombinu ni kujitia umasikini na kujibadili kuwa kibarua katika ardhi yako mwenyewe uliyoimiliki kabla ya kuiuza.”
Chongolo ameongeza: “maeneo yote niliyokuwa nawakuta Wagogo hapo wamesongezwa Ntyuka huko, kwanini mnauza ardhi kwa bei ya kutupa, bakieni na ardhi katikati ya Dodoma, kama ilivyo watanzania wengine na ninyi (Wagogo) hapa ndio nyumbani, acheni kuachia ardhi mtabadilika kuwa vibarua wa watu ambao wamenunua ardhi kwenu na wamebadili kuwa wafanyakazi wao.”
Ziara hiyo ya siku 8 yenye lengo la kukagua na kuhimiza utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025 pamoja na kuimarisha uhai wa Chama katika mkoa wa Dodoma itahitimishwa kwa mkutano mkubwa utakaofanyika tarehe 25, Juni 2023 katika uwanja wa Mtekelezo, Dodoma mjini.
Katika ziara hiyo Katibu Mkuu Chongolo ameongozana na Wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Ndugu Sophia Mjema na Katibu wa NEC Oganaizesheni Ndugu Issa Haji Ussi Gavu.