Na Immaculate Makilika – MAELEZO
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa katika mtandao wa www.tanzaniaweb.com Machi 3, 2023, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasilino Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Bakari anasema kuwa, hadi takwimu za mwezi Januari 2022 ni asilimia 27 ya Watanzania ndio wanaomiliki simu janja na kuwa malengo ya Serikali ni kuhakikisha watumiaji wa simu janja wanafikia 100%.
Ni wazi kwamba programu ya WhatsApp imezidi kuwa bora ili kuendelea kuwafurahisha watumiaji wake. Wengine husema bora ukose programu zingine kwenye simu lakini si WhatsApp.
WhatsApp imekuwa zaidi ya sehemu ya kuwasiliana na kutumiana jumbe zenye kufurahisha, lakini pia ni fursa ya kibiashara kwa wajanja. Watu wanataka kuuza au kujiweka karibu na wateja wao. Wengine ndio kwanza wanafungua biashara zao wakitafuta namna ya kujitangaza. Hivyo ni sawa kusema WhatsApp imekuwa kimbilio la wajasiriamali wengi wa Kitanzania.
Watu wameanzisha makundi sogozi ya WhatsApp kwa lengo la kuendesha semina na mafunzo mbalimbali. Kuendesha vikundi vya kukopeshana, maarufu kama ‘vikoba’. Vilevile makundi haya yanatumika kuhamasisha watu kujumuika kwenye matamasha na warsha mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukutanisha marafiki wa siku nyingi.
Siku za hivi karibuni si ajabu hata vikao vya Sendoff na harusi vinaendeshwa kwenye makundi ya WhatsApp. Na hivyo progamu hii ya WhatsApp imekuwa njia rahisi ya kuwafikia watu kwa muda mfupi ndio maana katika Mkoa wa Mara hasa wataalamu wa afya wameamua kutumia progamu hii hasa kundi sogozi ili kurahisisha utoaji huduma za haraka kwa wagonjwa na hivyo kukoa maisha ya wengi.
Aidha, Serikali imejenga na kuusambaza Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambao ndio njia kuu ya upatikanaji wa huduma mawasiliano ya simu na intaneti nchini ili wananchi na taasisi zote za umma ziweze kupata huduma za mawasiliano ya uhakika kwa gharama nafuu.
Kupitia uwekezaji huo wa Serikali unaoendelea kufanywa katika maeneo mbalimbali nchi nzima, umekuwa ukitoa fursa kwa wakazi wa Mkoa wa Mara na hasa katika maeneo ya Musoma Mjini wa kutumia simu janja na hususan mtandao wa WhatsApp katika kutoa taarifa za gafla za wagonjwa kabla ya kufikishwa hospitalini ili waweze kupatiwa matibabu.
Akizungumza katika mahojiano maalum hivi karibuni na mwandishi wa makala hii, Mkuu wa Idara ya Mama na Uzazi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara maarufu kama Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyojengwa katika eneo la Kwangwa, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Mama na Mtoto, Patrick Kenguru anasema kuwa kwa kawaida wagonjwa 10 hadi 15 hujifungua kwa siku na kuwa hapo baadae hospitali hiyo itaweza kuwahudumia akina mama wengi zaidi watakaoenda kujifungua kutoka Kanda ya Ziwa na mikoa ya jirani kwa kuwa vifaa vya kisasa vipo.
Aidha, Dkt. Kenguru anaeleza kuwa kwa mwezi wanahudumia wagonjwa 300 hadi 400, hivyo wameweza kupunguza vifo vya mama na mtoto ambapo hapo awali akina mama walikuwa wanatumia zaidi mitishamba na hivyo kupelekea vifo.
“Tunatumia kundi sogozi la WhatsApp (MPSDR Group) kupata taarifa za wagonjwa na hivyo tunawasaidia kutibu na kuokoa maisha, kwa Mkoa huu wa Mara ambapo kuna wataalamu wa afya tunatumia kundi sogozi kupeana taarifa za dharula za wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa,” anasema Dkt. Kengeru.
Anaendelea kusimulia, “mfano mgonjwa wa pembezoni anatoa taarifa na tunaandaa utaratibu na kuanza kumhudumia mgonjwa akiwa njiani kwa kuwasiliana na wataalamu wa afya waliopo maeneo ya karibu na mgonjwa kwa kumpa huduma ya kwanza na hivyo kupitia kundi hili tumefanikiwa kupunguza vifo vya mama na mtoto kabla ya mgonjwa hajafika hospitali”.
Charles Manumbu ni mkazi wa eneo la Kwanga mkoani Mara anasema, “Huduma alizopata mke wangu zilikuwa nzuri sana, tunashukuru wahudumu wa hospitali hii. Lakini pia mimi nilipata kazi wakati wa ujenzi wa hii hospitali kwa kweli tunaishukuru Serikali kwa kuleta miradi na kusaidia vijana tunanufaika kwa kupata kipato na hivyo kutunza familia zetu lakini pia kusogeza karibu huduma za afya”.
Naye, Mgeta Masatu mkazi wa Musoma anaeleza, “Hospitali hii imeanza kutoa huduma za mama na mtoto, kwa kweli shida iliyokuwepo awali ni kutokuwa na hospitali karibu na hivyo ilitulazimu sisi kutumia gharama kubwa kupata huduma hizi lakini pia wakati mwingine kusababisha vifo vya akina mama wajawazito, namshukuru Mhe. Rais kwa kutupa huduma hii mkoani Mara.
Hospitali hii ya Rufaa ya Mkoa wa Mara inatajwa kuwa na vifaa vya kisasa na wataalamu wabobezi katika kutoa huduma za mama na mtoto.
Muuguzi Kiongozi wa Kitengo cha Kangaroo Mothercare, Anastella Ishengoma anathibitisha hilo kwa kusema wamekuwa wakihudumia wanawake wajawazito kutoka maeneo mbalimbali kwa kutumia vifaa bora vya kusaidia kukuza watoto wanaozaliwa kabla ya wakati yaani njiti na hivyo kuwa mkombozi kwa wanawake wengi wa mkoa huo.