Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
MKUU wa mkoa wa Pwani, alhaj Abubakari Kunenge ameiagiza Halmashauri ya Bagamoyo,kuhakikisha inayaendeleza maboma ya miradi iliyokwama yenye thamani ya Bilioni 1.2 ,kwani kwa kuendelea kubaki viporo ni hasara kwa Serikali.
Aidha ,ameitaka Halmashauri hiyo kutumia raslimali zilizopo kwenye uchumi wa bluu na historia za kale ili kukuza Uchumi wake ambao bado unatakiwa kufanyiwa kazi maalum.
Kunenge alitoa maagizo hayo katika kikao cha Baraza la halmashauri maalum la kupitia hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Kunenge alieleza ,agizo hilo sio kwa Halmashauri ya Bagamoyo pekee bali kila Halmashauri ya mkoa huo ,zijipange kukamilisha miradi yote viporo ili ilete tija ndani ya jamii.
Alielezea,kupata hati safi kuendane na utekelezaji wa vipaombele vyenye tijà vitakavyotatua kero za wananchi pamoja na kukamilisha miradi iliyotengewa mabilioni ya fedha kutoka Serikalini.
“Miradi inakuja kuleta jibu kwa Wananchi, miradi ya toka mwaka 2015 ,haijakamilika hadi leo,hii ni hasara kwa Serikali,tengeni fedha za mapato ya ndani kukamilisha baadhi ya miradi hii, mkiiacha miradi Kuwa maboma mnachelewesha maendeleo ya wananchi,” Naziagiza Halmashauri zote kutekeleza miradi hiyo ya wananchi ilete tija badala ya kujivunia hati safi kila mwaka “alisisitiza Kunenge.
Vilevile, Kunenge alimuagiza Katibu Tawala mkoa wa Pwani, Rashid Mchatta pamoja na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, kufanya kazi maalum kwani kuna fursa nyingi kwenye uchumi wa bluu na kutumia historia za kale ili kujiinua kimapato.
” Bagamoyo Ina fursa za kihistoria ,uchumi wa bluu ,lakini bado inahitajika nguvu ya kufanyia kazi madhubuti kuinua uchumi uliopo .”
Mkuu huyo wa mkoa, alihimiza kutafuta vyanzo vipya vya mapato na kufanyia uchambuzi vyanzo vilivyopo ambavyo havifanyi vizuri kuongeza mapato ili visimamiwe na kuwekewa nguvu viweze kufanya vizuri.
“Tafuteni vyanzo vipya vya mapato. Nawaagiza watendaji wa Halmashauri kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ili kuisaidia Serikali kutimiza majukumu yaliyopo kwa wakati”
Mkaguzi Mkuu wa nje kutoka ofisi ya CAG Mkoa wa Pwani Mary Dibogo alieleza ,Halmashauri zihakikishe zinaepuka kuzalisha hoja.
Alizitaka pia zikamilishe miradi ya kipindi kirefu ikiwemo wilaya ya Bagamoyo ambayo haijakamilisha miradi yenye thamani ya Bilioni 1.2, sanjali na Chalinze miradi yenye thamani ya Bilioni 2.3 na Kisarawe miradi iliyoanzishwa haijakamilishwa ya Bilioni 2.2.
Dibogo alisema, fedha zinatengwa na Serikali ili kutekeleza miradi na kama ikiwa haitoshelezi Lazima ipatiwe namna ya kuikamilisha .
Awali Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo Mohammed Usinga alieleza, kulikuwa na hoja 35, kati ya hizo 18 zimefutwa na 17 bado hazijafungwa.
Usinga alimuhakikishia ,mkuu wa mkoa wa Pwani kwamba, Halmashauri hiyo itafanyia kazi maagizo na maelekezo yote.