Basi la Kampuni ya Newforce lenye namba za usajili T. 173 DZU lililokuwa likitokea jijini Dar es Salaam kuelekea mkoani Rukwa limepata ajali katika eneo la kijiji cha Igando mkoani Njombe na kusababisha vifo vya watu watano huku watu kadhaa wakijeruhiwa.
Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Njombe John Imori mpaka sasa wamethibitisha vifo vya watu watano (wanaume wanne na mtoto wa kike mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 8/ 9).
“Kwa sasa tumebaini vifo hivi vya watu watano lakini bado idadi ya majeruhi hatujaipata hivyo tutaendelea kutoa taarifa zaidi kwa kadri tunavyoendelea na zoezi hili. Kwa sasa juhudi za uokoaji zinaendelea”,amesema Kamanda Imori.
Amekitaji chanzo cha ajali hiyo kuwa ni Basi la Newforce lilikuwa likijaribu kulipita lori lililokuwa mbele yake matokeo yake likaacha njia na kugonga daraja na kisha kutumbukia mtaroni.